Ad
Breaking🔥

LUKUMAY AONGOZA HARAMBEE YA MILIONI 100

LUKUMAY: UIMBAJI NI SEHEMU YA MAISHA YA BINADAMU

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, amesema uimbaji ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu, ukitumika kama njia ya kuwasilisha hisia, kupata faraja, kuunganisha jamii na kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Dkt Lukumay ameyasema hayo leo Septemba 27,2026 wakati akiwa mgeni rasmi katika harambee na uzinduzi wa Albamu ya Kwaya ya Mwangaza, iliyofanyika katika Kanisa la DNPC Engedi-Ngaramtoni, mkoani Arusha ambapo hitaji la harambee hiyo ni sh,milioni 100.


Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt Lukumay alisema muziki haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa biashara na kipato pekee, bali ni sehemu ya maisha ya mwanadamu ambayo imekuwepo tangu enzi za mababu na imekuwa ikitumika katika mazingira mbalimbali ya kijamii na kiroho.

“Muziki ni sehemu ya maisha ya binadamu. Wimbo na muziki si kwa ajili ya kupata kipato pekee, bali ni namna ya mwanadamu kuwasilisha hisia zake. Mtu anapokuwa na mambo makubwa moyoni, anaweza kuimba na kupata faraja,” alisema.

Alisema urithi wa kuimba umeendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine, akirejea Biblia inayomtaja Yubali kuwa mmoja wa watu wa mwanzo kutajwa katika historia ya wapiga kinanda na filimbi.

Dkt Lukumay alisema umuhimu wa muziki unaonekana pia katika uwezo wake wa kuwasaidia watu kueleza hisia zao, iwe ni wakati wa furaha, huzuni, changamoto au katika kumshukuru na kumtumikia Mungu.

“Watu wana mambo makubwa katika mioyo yao na njia mojawapo ya kuwasilisha hisia hizo na kuleta faraja ni kuimba. Ndiyo maana tunapaswa kutambua umuhimu wa muziki katika maisha yetu,” alisema.

AWASHUKURU WAUMINI KWA MAOMBI



Katika hafla hiyo, Dkt Lukumay aliwashukuru Askofu na waumini wa Kanisa la DNPC Engedi-Ngaramtoni kwa kumwalika kuwa mgeni rasmi, akisema kanisa hilo limekuwa sehemu ya kumuombea katika safari yake ya kisiasa.

Alisema alipowahi kufika katika kanisa hilo, waumini walimuombea ili ashinde uchaguzi na kuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, akisema anaendelea kuthamini maombi hayo.

“Nilipokwenda mara ya kwanza katika kanisa hili, waumini mliniombea na kuhakikisha kwamba nitashinda uchaguzi. Kupata ubunge wa Arumeru Magharibi ni sehemu ya sala kubwa mlizoniombea. Nawashukuru sana,” alisema.

Dkt Lukumay aliomba pia kanisa hilo kuendelea kuiombea familia yake, hususani mke wake, Natasha Dawaki, ambaye alisema amekuwa akimuombea na kumuunga mkono katika safari yake ya kisiasa.

Alisema mke wake amekuwa akishiriki katika maombi na kufunga kwa ajili ya kumuomba Mungu amsaidie kufanikisha azma yake ya kuwa mbunge.

ALIVYOSAIDIA MTOTO KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO

Katika hatua nyingine, Dkt Lukumay alieleza kisa cha mtoto mmoja kutoka Arumeru Magharibi aliyekuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo, akisema msaada ulipatikana baada ya kijana Emmanuel kuanzisha harambee kupitia makundi ya kijamii.

Alisema familia ya mtoto huyo ilikuwa na hali ngumu kiuchumi na ilihitaji takribani Sh9 milioni kwa ajili ya matibabu, lakini juhudi za Emmanuel ziliwezesha wananchi kuchangia zaidi ya Sh1.1 milioni.

Dkt Lukumay alisema baada ya kufuatilia suala hilo aligundua kuwa mtoto huyo anatoka katika Jimbo la Arumeru Magharibi, hivyo alishiriki katika juhudi za kumsaidia mpaka alipofanyiwa upasuaji wa moyo.

“Nilifika kwenye lile boma na kweli nikawakuta watu maskini, lakini wenye upendo mkubwa wa Mungu. Tukamchukua mtoto na kumpeleka hospitalini, akafanyiwa upasuaji wa moyo. Wazazi wake wamenishukuru,” alisema.

Alisema tukio hilo linaonyesha nguvu ya mshikamano wa jamii katika kusaidia watu wenye mahitaji, huku akiwashukuru wote walioshiriki katika kumsaidia mtoto huyo.


Akihitimisha hotuba yake, Dkt Lukumay alisema uzinduzi wa Albamu ya Kwaya ya Mwangaza ni sehemu ya kumtukuza Mungu na kuendeleza vipaji vya vijana.

“Tulikuja kuzindua wimbo, lakini ninapoona kijana mdogo anayependa kuimba, ni lazima tumuunge mkono. Leo tutaimba pamoja, Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa kuwa amefanya mambo ya ajabu,” alisema

ends.

Post a Comment

Previous Post Next Post