Ad
Breaking🔥

KABUDI ATAKA SERIKALI IPIMWE KWA MABADILIKO YA WANANCHI KIUCHUMI

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema mafanikio ya Serikali hayapaswi kupimwa kwa idadi ya shughuli, mikutano au nyaraka zinazotekelezwa, bali kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Profesa Kabudi alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Mwinyi, wakati wa kufunga Kongamano la Tano la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza, lililopitisha maazimio 10 ya kuimarisha matumizi ya ushahidi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.


Alisema ufuatiliaji na tathmini vinapaswa kuwa sehemu ya kawaida ya utendaji wa Serikali na menejimenti za taasisi, kwa kuwa vinasaidia kupima matokeo, kubaini changamoto mapema na kufanya maamuzi yanayozingatia ushahidi.

“Wananchi ndio kipimo cha mwisho cha matokeo yetu. Tathmini ni mfumo wa mrejesho unaotusaidia kufahamu nani amefikiwa, nani hajaafikiwa, huduma zimeboreshwa kwa kiwango gani na hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa,” alisema.

Profesa Kabudi alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mfumo imara wa ufuatiliaji, tathmini na kujifunza utakaowezesha Serikali kupima kwa wakati iwapo malengo, shabaha na viashiria vilivyowekwa vinafikiwa.

Alisema wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya menejimenti za taasisi, kwa kutoa ushauri wa kitaalamu, kuhakiki taarifa, kubaini changamoto na kusaidia kufanya maboresho.

Aliwataka viongozi kuhakikisha taarifa zinazozalishwa na mifumo hiyo zinasomwa, kujadiliwa na kutumika katika kufanya maamuzi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na makundi yenye mahitaji maalumu.

Kabudi alisema maazimio yaliyopitishwa katika kongamano hilo hayapaswi kubaki kuwa kumbukumbu, bali yanapaswa kutafsiriwa katika mipango ya utekelezaji yenye hatua mahsusi, wahusika, muda na viashiria vya kupima maendeleo.

Alisema pia ni muhimu kuwepo kwa utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa maazimio na maelekezo yaliyotolewa.

Katika kongamano hilo, jumla ya mawasilisho zaidi ya 36 yalifanyika, yakiwamo 11 ya wazungumzaji wakuu na zaidi ya 26 yaliyowasilishwa katika makundi.

Kwa upande wake, Dkt. Rogers Lumenyera, aliyewasilisha maazimio kwa niaba ya washiriki, alisema kongamano hilo limepitisha maazimio 10 ambayo utekelezaji wake utapimwa katika kongamano lijalo mwaka 2027.

Alisema kongamano hilo la siku tano limewakutanisha washiriki 594 kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, pamoja na wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika.

Miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa ni kuharakishwa kwa uundaji wa Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na mkataba wake wa utekelezaji, ili kuweka mwongozo wa pamoja wa kuratibu na kusimamia shughuli hizo nchini.

Azimio jingine ni kukamilishwa kwa mfumo jumuishi wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini utakaoanishwa na mifumo mingine ya Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.

Washiriki pia walitaka taarifa za ufuatiliaji na tathmini zitumike katika kufanya maamuzi, kuboresha utekelezaji wa mipango na kufuatilia hatua za maboresho.

Taasisi za umma zimetakiwa kuimarisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini kwa kuviwezesha kwa watumishi wenye ujuzi, rasilimali na vifaa, huku zikitenga fedha mahsusi kwa shughuli hizo.

Katika eneo la vijana, Serikali, taasisi binafsi na wadau wengine wametakiwa kuwapa nafasi katika mafunzo, mazoezi kwa vitendo, ushauri wa kitaaluma na kazi za ufuatiliaji na tathmini ili kujenga kizazi kipya cha wataalamu.

Wataalamu wa sekta hiyo pia wametakiwa kuendelea kujenga uwezo na kutumia teknolojia katika ukusanyaji, uchakataji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa, kwa kuzingatia usalama, usiri na maadili ya kitaaluma.

Aidha, Chama cha Wataalamu wa Tathmini Tanzania (TAEA) kimetakiwa kushirikiana na Serikali na taasisi za mafunzo kuandaa Muundo wa Umahiri katika Taaluma ya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E Competency Framework).

Azimio jingine linataka kuandaliwa kwa mafunzo mahsusi kwa viongozi katika ngazi mbalimbali, ikiwamo kamati za Bunge zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini, ili kuongeza uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Dkt. Lumenyera alisema maazimio hayo yanalenga kuhakikisha ufuatiliaji na tathmini hauishii katika ukusanyaji wa taarifa, bali ushahidi unaozalishwa unatumika kuboresha maamuzi, sera, mipango, bajeti na huduma kwa wananchi.

“Tumeazimia maazimio haya ili yafanyiwe kazi na tutakapokutana katika kongamano la mwaka 2027, tutajipima kuona tumefikia wapi katika utekelezaji wake,” alisema.

Profesa Kabudi aliipongeza menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAEA, taasisi za Serikali, elimu na utafiti, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa kushiriki katika kongamano hilo.

Alisema juhudi hizo ni sehemu ya kujenga utamaduni wa Serikali unaotumia ushahidi katika kufanya maamuzi na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.


Ends..


Post a Comment

Previous Post Next Post