Ad
Breaking🔥

KIHONGOSI: UONGOZI HAUCHUKULIWI KWA VURUGU

KIHONGOSI: UONGOZI HAUCHUKULIWI KWA VURUGU

Na Hadija Bagasha | Tanga


KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema uongozi wa nchi haupatikani kwa vurugu wala kwa kukwepa uchaguzi, akisisitiza kuwa sanduku la kura ndilo njia ya wananchi kuamua viongozi wao.

Kihongosi amesema hayo jana, Septemba 25, 2026, wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.

Amesema Tanzania ina utaratibu wa kuchagua viongozi kila baada ya miaka mitano, hivyo mtu au chama kinachotaka kushika madaraka kinapaswa kushiriki mchakato wa uchaguzi na kuwaomba wananchi ridhaa kupitia kura.

“Uongozi hauchukuliwi kwa vurugu, uongozi unachukuliwa kwa kwenda kupigiwa kura. Huwezi ukasema hushiriki uchaguzi halafu upate uongozi. Haiwezekani,” amesema.

Amesema tofauti za kisiasa hazipaswi kutumiwa kama sababu ya kuvuruga amani na utulivu wa nchi, akiwataka wananchi kuwa makini na watu wanaowahamasisha kuingia katika maandamano au vurugu huku wao wakibaki pembeni.

“Msikubali kushawishiwa na watu wachache kuandamana na kuharibu amani ya nchi, halafu wao wabaki pembeni huku wananchi mkiumia,” amesema.

Kihongosi amesema amani ni msingi wa shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo wananchi wana wajibu wa kuilinda na kutoruhusu mtu yeyote kuvuruga utulivu uliopo. Kauli yake kuhusu umuhimu wa wananchi kutokubali kutumiwa katika vurugu imekuwa sehemu ya ujumbe wake katika ziara zake za hivi karibuni.

Amesema Tanzania inaongozwa kwa misingi ya Katiba, sheria na taratibu zilizowekwa, hivyo hakuna mtu anayepaswa kufanya anavyotaka kwa kisingizio cha tofauti za kisiasa.

“Hatuwezi kuruhusu watu wafanye wanavyotaka ndani ya nchi hii. Hii si klabu ya pombe kwamba kila mmoja anakunywa na kufanya anachotaka. Taifa linaongozwa kwa misingi ya sheria, Katiba na taratibu zinazoliongoza Taifa,” amesema.

AITETEA CCM KWA MIRADI

Kuhusu utekelezaji wa ahadi za kisiasa, Kihongosi amesema CCM imeendelea kupata uungwaji mkono kutokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, akitolea mfano huduma ya umeme vijijini.

“Chama kilisema kitapeleka umeme vijijini na kweli umeme unawaka. Mnazo saluni, mnayatengeneza madirisha na mageti na mambo mengine. Hatusimuliwi, tunajionea wenyewe,” amesema.

Amesema wananchi wanapaswa kupima ahadi za kisiasa kwa kuangalia utekelezaji wake, huku akizitaka pande zote zinazoshiriki siasa kuheshimu taratibu za uchaguzi na sheria za nchi.

Katika ziara hiyo, Kihongosi pia ametaja changamoto ya upatikanaji wa maji Mkinga na kusema Serikali imetenga Sh35 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji katika eneo hilo.

TANGA YATAJA MIRADI

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abrahman Abdallah, amemuomba Kihongosi kufikisha salamu kwa Rais, akisema wananchi wa mkoa huo wanaendelea kushuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rajab amesema baadhi ya miradi hiyo imefanyika kwa kiwango kikubwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga, akisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kushughulikia mahitaji ya wananchi.

“Tunakushukuru sana kwa kutenga muda wako na kufika Mkoani Tanga,” amesema.

Ziara ya Kihongosi mkoani Tanga inalenga kukagua uhai wa CCM, kusikiliza wananchi na wanachama wa chama hicho, pamoja na kuzungumzia masuala ya maendeleo, amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post