TASAC YASISITIZA MAZOEZI YA MARA KWA MARA KUOKOA MAISHA BAHARINI
Na Hadija Bagasha | TANGA
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesisitiza umuhimu wa kuwa na utayari wa kudumu wa utafutaji na uokoaji baharini, likisema mazoezi ya mara kwa mara ni muhimu katika kuhakikisha maisha yanaokolewa kwa wakati wakati wa ajali au dharura kwenye usafiri wa majini.
Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Kapteni Mussa Mandia, aliyasema hayo jana mjini Tanga wakati wa zoezi la majaribio la utafutaji na uokoaji baharini lililolenga kupima utayari na uwezo wa taasisi pamoja na wadau mbalimbali katika kukabiliana na dharura za majini.
Mandia alisema zoezi hilo limeonesha umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo mipango, kanuni na taratibu za utafutaji na uokoaji, akisisitiza kuwa kuwa na vifaa vya uokoaji pekee hakutoshi bila kuwa na wataalamu wenye ujuzi, uzoefu na utayari wa kuchukua hatua kwa haraka.
“Zoezi la leo linaonesha kauli mbiu kwa vitendo. Kanuni, mipango na vifaa vya uokoaji vinakuwa na thamani kubwa zaidi pale tunapovifanyia mazoezi na kuhakikisha watu wetu wapo tayari kuchukua hatua wakati wa dharura, kama ambavyo tumejionea,” alisema.
Alisema Tanzania inatambua wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa watu wanaotumia usafiri wa majini, ikiwa ni pamoja na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Utafutaji na Uokoaji Baharini wa mwaka 1979 pamoja na mikataba mingine 23 ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO).
Kwa mujibu wa Mandia, utekelezaji wa wajibu huo hauishii katika kuwa na sera, kanuni na vifaa vya uokoaji, bali unahitaji maandalizi ya kila siku, mifumo madhubuti ya mawasiliano, wataalamu wenye ujuzi na vyombo vya uokoaji vinavyotunzwa na kuwa katika hali nzuri ya kufanya kazi.
Alisema pia ushirikiano wa karibu miongoni mwa taasisi na wadau wanaohusika na usalama wa majini ni muhimu katika kuhakikisha taarifa za dharura zinawasilishwa na hatua za uokoaji zinachukuliwa kwa wakati.
Mandia alisema umuhimu wa utayari huo unaongezeka zaidi mkoani Tanga kutokana na shughuli kubwa za usafirishaji wa abiria na mizigo zinazofanywa kwa kutumia vyombo mbalimbali vya majini, kuanzia vyombo vidogo hadi meli kubwa zinazofanya safari ndani na nje ya Tanzania.
“Tunapofanya mazoezi ya pamoja tunajifunza namna ya kutoa taarifa za dharura, kuratibu muitikio na kuwaokoa watu kwa wakati ili kuepusha hatari kubwa zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa mazoezi hayo pia yanaipa fursa taasisi zinazohusika kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa operesheni za utafutaji na uokoaji na kuzifanyia kazi kabla ya kutokea kwa dharura halisi.
Alisema TASAC itaendelea kusisitiza ushirikiano wa wadau wote katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, huku mazoezi ya mara kwa mara yakitumika kujenga uwezo wa mifumo ya uokoaji kuitikia kwa haraka na kwa ufanisi pale maisha ya watu yanapokuwa hatarini.
Ends



Post a Comment