TANZANIA, ALGERIA ZAFUNGUA MILANGO YA USHIRIKIANO SEKTA TANZANIA
...Dawa, nishati, elimu, kilimo na ufugaji wa nyuki zaimarishwa
Na Arusha Digital | ALGIERS
Hatua hiyo imeelezwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Algeria katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers jana.
Balozi Matinyi alisema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa nchi hizo mbili, ambao wameelekeza kwamba baada ya kutambua maeneo ya kimkakati ya ushirikiano, hatua inayofuata ni kuhakikisha ushirikiano huo unazaa matokeo yanayowanufaisha wananchi wa Tanzania na Algeria.
Alisema wakati akiwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, Juni 10, 2026, alielezwa umuhimu wa kuufanya ushirikiano huo kuwa wa vitendo.
“Nilipowasilisha hati zangu za utambulisho mnamo Juni 10, 2026, Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kwamba sasa umefika wakati wa kuuweka ushirikiano wetu katika vitendo. Nilipokuja Algeria, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan naye alisisitiza kwamba kutokana na ushirikiano wetu wa kimkakati, sasa ni wakati wa kupata manufaa kwa ajili ya wananchi wetu,” alisema.
DAWA: ALGERIA KUTUMA WATAALAMU TANZANIA
Katika sekta ya viwanda vya dawa, Balozi Matinyi alisema Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) pamoja na kampuni ya dawa ya Serikali ya Algeria, Saidal Group, zinatarajia kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Oktoba 2026.
Alisema ziara hiyo itafanyika kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), kwa lengo la kujadili maeneo ya ushirikiano wa kitaalamu na uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Balozi Matinyi, ushirikiano huo una fursa kubwa kutokana na uwezo wa nchi zote mbili katika sekta ya dawa.
Alisema Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha juu cha ML3 katika mfumo wa ukaguzi wa dawa mwaka 2018, kwa mujibu wa tathmini ya kimataifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), huku Algeria ikiwa na sehemu kubwa ya viwanda vya dawa barani Afrika.
“Kwa msingi huo, nchi hizi mbili zinaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi kupitia kubadilishana utaalamu, teknolojia na uwekezaji,” alisema.
Aidha, alisema kampuni ya dawa ya Hikma iko katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya ushirikiano wa biashara na uwekezaji na kampuni tanzu ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Medipharm, kwa lengo la kuhudumia masoko ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Alisema kampuni nyingine ya Algeria, Frater Razes, nayo inatarajia kuwasili Tanzania mwezi Oktoba kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu uwekezaji na biashara katika sekta ya dawa.
NISHATI: TANZANIA YAFUNGUA MAZUNGUMZO NA SONELGAZ
Katika sekta ya nishati, Balozi Matinyi alisema Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ilifanya ziara nchini Algeria mwezi Julai 2026.
Alisema ziara hiyo ililenga kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiufundi pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta ya umeme.
Wajumbe hao walitembelea maeneo mbalimbali ya kiufundi ya Shirika la Umeme na Gesi la Algeria, SONELGAZ, pamoja na kiwanda cha vifaa vya umeme cha GISB Electric.
ELIMU: WANAFUNZI 150 KUNUFAIKA NA MASOMO ALGERIA
Katika sekta ya elimu ya juu, Balozi Matinyi alisema Algeria imetoa nafasi 176 za masomo ya juu kwa wanafunzi kutoka Tanzania.
Alisema Serikali ya Tanzania imeamua kuchagua wanafunzi 150 wenye ufaulu wa juu watakaonufaika na nafasi hizo kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.
Alisema wanafunzi hao watasomea zaidi katika maeneo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba, ambayo ni miongoni mwa nyanja muhimu katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi kwa maendeleo ya taifa.
KOROSHO: KAMPUNI YA ALGERIA YAINGIA MTWARA
Katika biashara ya mazao ya kilimo, Balozi Matinyi alisema kampuni ya Algeria, Sarl Anacard’Or, imechukua hatua ya kununua ghala la kuhifadhia korosho mkoani Mtwara kwa ajili ya kuwezesha ununuzi na usafirishaji wa zao hilo kwenda Algeria.
Alisema kampuni hiyo pia ipo katika hatua za kukamilisha mipango ya kuanzisha shughuli za ubanguaji wa korosho nchini Tanzania, hatua inayoweza kuongeza thamani ya zao hilo kabla ya kufikia soko la kimataifa.
Aidha, alisema kampuni nyingine ya Algeria, CAM Sarl, inayotengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo, dawa na vifaa vya kufungashia, imekubali kushirikiana na Tanzania katika upatikanaji wa teknolojia na mashine hizo.
Kwa mujibu wa Balozi Matinyi, ushirikiano huo unalenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo nchini kabla ya kupelekwa katika masoko ya dunia.
UFUGAJI WA NYUKI WAFUNGUA UKURASA MPYA
Balozi Matinyi alisema Tanzania na Algeria pia zimeanza maandalizi ya kuanzisha ushirikiano katika sekta ya ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa mazao yatokanayo na sekta hiyo.
Alisema hatua hiyo imefuatia ziara ya maafisa na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na wadau wa sekta binafsi nchini Algeria mwezi Septemba 2026.
Alisema katika ziara hiyo, wataalamu wa Tanzania na Algeria walikubaliana kuanza kushirikiana katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu.
ALGERIA YAVUTIWA NA FURSA ZA UTALII TANZANIA
Akihitimisha mazungumzo yake na waandishi wa habari wa Algeria, Balozi Matinyi aliwaalika wananchi wa Algeria kutembelea Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Alivitaja vivutio hivyo kuwa ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, pamoja na fukwe za Zanzibar.
Alisema Tanzania ina fursa mbalimbali zinazoweza kuwavutia watalii kutoka Algeria na kuongeza zaidi mahusiano ya watu kwa watu kati ya mataifa hayo mawili.
Algiers, Algeria | Septemba 30, 2026
Ends

إرسال تعليق