ALICIA MALLY ADAI KUPIGWA NA ISAYA DOITA, MENO MATATU YAVUNJIKA
..Asema alinusurika kifo, apata majeraha kichwani na mwili mzima, adai kuvuliwa nguo mbele ya watoto
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Amesema mbali na meno matatu kuvunjika, amepata majeraha kichwani na mwili wake wote una majeraha, hali ambayo imemlazimu kupata matibabu na kufanyiwa vipimo zaidi hospitalini.
Kwa mujibu wa Alicia, tukio hilo lilitokea nyumbani usiku wa kuamkia leo baada ya kutokea mabishano kati yake na Doita, kabla hali hiyo kubadilika na kuwa shambulio la kimwili baada ya mke kumfungulia geti na kuingia ndani.
“Alianza kunipiga ngumi mpaka nikaanguka chini. Nilipokuwa chini akaanza kunikanyaga na kunipiga kwa miguu. Nilipiga kelele kwa sababu nilikuwa napigwa sana,” amedai Alicia.
Amesema kipigo hicho kilikuwa kikali kiasi kwamba alihofia kupoteza maisha, huku akieleza kuwa baada ya kuanguka chini aliendelea kupigwa na kukanyagwa.
Alicia amesema baada ya tukio hilo alibaki na majeraha sehemu mbalimbali za mwili pamoja na majeraha kichwani.
Amesema bado anapata maumivu na hali yake inahitaji uangalizi wa madaktari, huku akieleza kuwa amepewa matibabu ya awali na kuendelea kusubiri vipimo na uchunguzi zaidi.
“Mpaka sasa bado nina maumivu. Mwili wangu wote umejeruhiwa na kichwani nimepata majeraha. Nimeambiwa nifanyiwe vipimo zaidi,” amesema.
DAI LA KUVULIWA NGUO MBELE YA WATOTO
Alicia pia amedai kuwa wakati wa tukio hilo alivuliwa nguo mbele ya watoto wake, ambao walikuwa wameamka na kushuhudia sehemu ya tukio.
Amesema baada ya watoto kuanza kulia, alijaribu kukimbilia chumba kingine ili kujiokoa, lakini anadai alifuatwa na kuendelea kupigwa.
Baadaye, amesema alifanikiwa kutoka nyumbani baada ya mmoja wa watoto wake kufungua mlango wa mbele, ndipo alipokimbia bila viatu akiwa anatokwa damu hadi kufika eneo la Msesaani.
Amesema alimuomba msaada mtu aliyekuwa akipita eneo hilo, ambaye baadaye alimsaidia kufika kituo cha polisi.
“NILINUSURIKA KUFA”
Alicia amesema tukio hilo limemfanya ahofie usalama wa maisha yake na kuiomba Serikali pamoja na vyombo vya dola kulichunguza suala hilo.
“Naomba Serikali iangalie tunavyonyanyasika. Kama watu hawana maelewano ndani ya nyumba, kuna kukaa na kuzungumza. Lakini adhabu ya kunipiga mpaka hali hii si sawa,” amesema.
Amesema alitoa taarifa polisi na kwamba Doita aliitwa kituoni, lakini baadaye aliachiwa, huku yeye akisema hajui hatua zaidi zilizochukuliwa.
DOITA: SIWEZI KUONGEA MASUALA YA NYUMBANI
Alipotafutwa na waandishi wa habari ili kupata upande wake kuhusu madai hayo, Isaya Doita alisema hawezi kuzungumza kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala yanayohusu familia yake.
Doita alisema suala hilo ni la nyumbani na hakutaka kulizungumzia kupitia vyombo vya habari.
Madai ya Alicia dhidi ya Doita bado ni tuhuma zinazohitaji uchunguzi wa vyombo husika na uthibitisho wa kitabibu.
Ends


إرسال تعليق