TANGA YAKUZA UCHUMI WA BAHARI, SERIKALI YAONYA UHIFADHI.
Na Hadija Bagasha, Tanga
Serikali imeonya kuwa kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi zinazotegemea bahari, mito na maziwa inapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira, ikieleza kuwa uharibifu wa rasilimali hizo unaweza kuhatarisha maisha ya wananchi, miundombinu na fursa zinazotokana na uchumi wa bluu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Ally Saidi Bakari, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi wa Zanzibar katika maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika Mkoa wa Tanga.
Mhandisi Ally amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za maji, ikiwemo bahari, mito na maziwa, zinazotoa fursa za ajira na kipato kupitia uvuvi, utalii, usafirishaji, biashara, kilimo cha mwani na shughuli nyingine za uchumi wa bluu.
Amesema fursa hizo zinahitaji kulindwa kutokana na changamoto zinazolikabili eneo la bahari, ikiwemo uharibifu wa mifumo ya ikolojia, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyozingatia uendelevu, akisisitiza kuwa maji ni msingi wa maisha na maendeleo ya jamii.
“Maji ni uhai, yawe baharini, mitoni au maziwa. Tusipoyaheshimu maji yatatushughulikia. Nguvu ya maji ni kubwa sana na tunapaswa kutambua umuhimu wake na kulinda rasilimali zilizopo,” amesema.
Ameonya kuwa kuendelea kuharibu mazingira ya bahari kunaweza kusababisha upotevu wa rasilimali, kuathiri maisha ya wananchi na kuongeza hatari kwa miundombinu na makazi yaliyopo maeneo ya mwambao.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ally, Tanzania inapaswa kutumia ipasavyo nafasi yake ya kuwa na bahari, mito na maziwa kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huku ikiweka mbele uhifadhi wa mazingira na usalama wa shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari na usafirishaji wa majini, akiwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi za kuboresha miundombinu hiyo.
Ametaja maboresho katika Bandari ya Zanzibar na Bandari ya Tanga pamoja na miundombinu ya usafirishaji katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kuwa sehemu ya hatua zinazolenga kuongeza matumizi ya rasilimali za maji katika kukuza uchumi.
TANGA YACHANGAMKA
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, amesema kuchaguliwa kwa Tanga kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kunatokana na nafasi ya kimkakati ya mkoa huo katika shughuli zinazotegemea bahari.
Mchatta amesema Tanga inaendelea kuwa kitovu cha uchumi wa bluu kutokana na shughuli za uvuvi, utalii, biashara, usafirishaji na uwekezaji unaohusisha matumizi ya rasilimali za bahari.
Amesema maboresho makubwa yanayofanyika katika Bandari ya Tanga yameanza kubadili kasi ya shughuli za kiuchumi mkoani humo, akibainisha kuwa idadi ya meli zinazofika bandarini hapo imeongezeka hadi kufikia takribani meli 17 kwa mwezi, kutoka meli moja kwa mwezi katika kipindi cha nyuma.
Amesema ongezeko hilo limefungua zaidi fursa za biashara na shughuli mbalimbali zinazozunguka bandari, huku miradi mikubwa ya kimkakati ikiongeza umuhimu wa Tanga katika uchumi wa taifa.
Miongoni mwa miradi hiyo ni bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, ambalo limeongeza shughuli za kiuchumi na kimkakati katika eneo hilo.
Hata hivyo, Mchatta amesema ongezeko la shughuli za bandari, uwekezaji na matumizi ya bahari linapaswa kuambatana na hatua madhubuti za kulinda mazingira ili rasilimali hizo ziendelee kuwa chanzo cha ajira, kipato na maendeleo kwa wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
USALAMA WA MAJINI WAPEWA UZITO
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ally ameitaka Serikali na taasisi zinazohusika na usafiri wa majini kuendelea kuimarisha usalama wa vyombo vinavyotumika baharini, mitoni na maziwani, kutokana na changamoto ya ajali za majini.
Amesema ukaguzi wa vyombo vya usafiri unapaswa kufanyika kabla na wakati wa matumizi ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali, akieleza kuwa maendeleo ya usafiri wa majini hayawezi kutenganishwa na usalama wa watumiaji.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yanatoa fursa kwa Serikali, wataalamu, wadau na wananchi kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kwa tija bila kuharibu mazingira.
Kwa Tanzania, ambayo ina mwambao wa Bahari ya Hindi pamoja na maziwa na mito mikubwa, uhifadhi wa mazingira ya maji unaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha shughuli za uvuvi, utalii, usafirishaji, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi zinaendelea kutoa fursa kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Mwisho.


Post a Comment