KIIR ABOMOA SERIKALI YA MPITO, ATEUA VIONGOZI WAPYA
Na Joseph Ngilisho | ArushaDigital
RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, amevunja Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa, wakati muda wa uongozi huo ukifikia ukomo, huku akiteua viongozi wa muda kuendesha shughuli za Serikali hadi kipindi cha uchaguzi mkuu.Hatua hiyo imekuja wakati Sudan Kusini ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa amani uliowakutanisha viongozi na makundi yaliyokuwa yakipigana nchini humo.
Baada ya kuvunja Serikali hiyo, Kiir ameteua viongozi wa muda kusimamia shughuli za Serikali, pamoja na magavana wa muda katika majimbo yote 10 na maeneo matatu ya kiutawala.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha shughuli za Serikali zinaendelea bila kuwepo kwa ombwe la kikatiba wakati nchi ikielekea katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2018, Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa ilipaswa kumaliza muda wake miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Serikali hiyo iliundwa Februari 22, 2020, kufuatia makubaliano ya amani yaliyolenga kumaliza mzozo wa kisiasa na mapigano yaliyokuwa yameikumba Sudan Kusini.
Hata hivyo, Septemba 2024, pande zilizohusika katika makubaliano hayo zilikubaliana kuongeza kipindi cha mpito kwa miaka miwili, hadi Februari 22, 2027, huku uchaguzi mkuu ukipangwa kufanyika Desemba 2026.
Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011, lakini baadaye ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2013 na kurejea kwa mapigano mwaka 2016.
Mzozo huo uliathiri kwa kiasi kikubwa mchakato wa ujenzi wa taifa na kusababisha juhudi mbalimbali za upatanishi na mikataba ya amani, ikiwamo makubaliano ya mwaka 2018 yaliyounda msingi wa Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa.
#ArushaDigitalUpdates#
Post a Comment