Ad
Breaking🔥

POLISI YAMTWANGA RISASI NJEMBA ALIYEVAMIA BENKI AKIOMBA PESA YA KULA

NJEMBA APIGWA RISASI NA POLISI BENKI ROCK CITY MALL

Na Joseph Ngilisho | MWANZ

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35 amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi, akidaiwa kuingia katika benki iliyopo ndani ya Rock City Mall, Mwanza, na kujaribu kuwanyang’anya silaha askari waliokuwa wakilinda benki hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, tukio hilo lilitokea Septemba 13, 2026, majira ya saa 7 mchana, ambapo mwanaume huyo ambaye hadi sasa utambulisho wake haujafahamika, aliingia katika benki hiyo akijifanya kuwa mteja.

Polisi imesema baada ya kuingia, mwanaume huyo alimtaka mhudumu wa benki ampatie fedha kwa ajili ya kula.

Mhudumu huyo alipomwelekeza taratibu za kufuata katika kutoa au kuweka fedha benki, mwanaume huyo aliendelea kusisitiza apewe fedha, hali iliyomfanya mhudumu kuhisi usalama wake uko hatarini na kwenda kuomba msaada kwa wafanyakazi wenzake.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwanaume huyo aliruka kaunta na kuelekea katika vyumba vya kuhesabia fedha, huku akimsukuma mhudumu na kuingia naye ndani.

Kitendo hicho kilisababisha taharuki miongoni mwa wafanyakazi na wateja waliokuwa ndani ya benki hiyo, ndipo askari waliokuwa wakilinda benki walipofika na kumtaka ajisalimishe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Polisi, mwanaume huyo alikaidi amri hiyo na kujaribu kuwanyang’anya askari silaha.

Katika hatua hiyo, askari walimdhibiti kwa kumpiga risasi iliyompata sehemu ya kiunoni kuelekea mguu wa kulia, na kusababisha jeraha lililovuja damu nyingi.

Polisi imesema mwanaume huyo alipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia akiwa njiani.

Mwili wake umehifadhiwa hospitalini kwa ajili ya taratibu za utambuzi na uchunguzi zaidi.

#ArushaDigitalUPDATES | Mwanza

.


Post a Comment

أحدث أقدم