Ad
Breaking🔥

BINTI MREMBO (24) AFARIKI KWA KUPIGWA CHUPA THE HUB CLUB ARUSHA

 BINTI MREMBO (24) AFARIKI KWA KUPIGWA CHUPA THE HUB CLUB ARUSHA

Na Joseph Ngilisho | Arusha

BINTI mwenye umri wa miaka 24, anayefahamika kwa jina la Irene, mkazi wa Mtaa wa Lemara, Kata ya Lemara jijini Arusha, amefariki dunia baada ya kudaiwa kujeruhiwa kwa chupa wakati akiwa pamoja na wenzake katika Klabu ya The HUB .

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu mazingira ya kifo hicho, huku Jeshi la Polisi likianza uchunguzi wa kina na kuwashikilia watu wawili waliokuwa pamoja na marehemu kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, mama mzazi wa Irene, Mariam Selemani, amesema marafiki wawili wa binti yake walifika nyumbani kwao jana, Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi na kumjulisha kuwa Irene alikuwa amejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Mariam amesema baada ya kufuatilia taarifa hiyo, alifika hospitalini na kubaini kuwa binti yake alikuwa amefariki dunia.

Hata hivyo, amesema maelezo aliyokuwa akipewa kuhusu mazingira ya tukio hilo yalitofautiana, jambo lililomfanya kutaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini kilichotokea.

“Awali niliambiwa kulikuwa na ugomvi, lakini baadaye nikaelezwa kuwa walipotoka hawakumuona Irene hadi walipomkuta amelala nje huku damu ikimtoka,” amesema Mariam.

Kwa upande wake, Rehema Ramadhan, aliyemlea Irene tangu akiwa mdogo, amesema marehemu alikuwa mtoto mwenye tabia njema na hakuwa na matatizo na watu.

Amesema familia imepokea taarifa ya kifo hicho kwa maumivu makubwa na kusisitiza umuhimu wa ukweli wa tukio hilo kubainika.

Baada ya kufika katika eneo la The HUB kwa ajili ya kupata maelezo zaidi, wafanyakazi walieleza kuwa meneja wa eneo hilo alikuwa kituo cha polisi.

Akizungumza kwa simu, Meneja Paulo amesema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 10, lakini amedai kuwa lilitokea nje ya geti la klabu hiyo.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku watu wawili waliokuwa pamoja na Irene wakishikiliwa kwa mahojiano kwa lengo la kusaidia kubaini mazingira yaliyopelekea kujeruhiwa na hatimaye kifo chake.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali wakati taratibu za mazishi zikiendelea.

End. 

Post a Comment

أحدث أقدم