Ad
Breaking🔥

NMB YAWEKA MKAKATI WA KUSHIRIKI DIRA 2050

NMB: SEKTA BINAFSI INJINI YA DIRA 2050

Na Joseph Ngilisho-ARUMERU

BENKI ya NMB imesema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikisisitiza kuwa mafanikio ya maendeleo yanapaswa kupimwa kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya wananchi, badala ya kuangalia kiasi cha fedha na rasilimali zilizotumika.

Kauli hiyo ilitolewa septembe 25,2026 na Meneja Mwandamizi wa Biashara za Serikali wa NMB, Josephine Kulwa, aliyemwakilisha Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa benki hiyo, Baraka Ladslaus, wakati wa ufungaji wa Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji Tanzania 2026,iliyofanyika katika hotel ya Ngurdoto nje kidogo ya jiji la Arusha ,wilayani Arumeru.

Kulwa alisema ushiriki wa NMB katika jukwaa hilo kama sehemu ya wadhamini wakuu wa mkutano huo, unatokana na kutambua umuhimu wa matumizi ya taarifa, ushahidi na matokeo ya tathmini katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.

“Maendeleo endelevu hayawezi kupimwa kwa ukubwa wa rasilimali tunazotumia pekee, bali kwa mabadiliko chanya ambayo rasilimali hizo zimeleta katika maisha ya watu,” alisema.

Alisema sekta binafsi, ikiwamo sekta ya fedha, ina wajibu wa kuwa kiungo kati ya rasilimali, mitaji na fursa za kiuchumi ili kuongeza uzalishaji, uwekezaji na ajira, huku ikiwafungulia wananchi nafasi zaidi za kushiriki katika uchumi.

Kwa mujibu wa Kulwa, NMB imeendelea kupanua huduma zake za kifedha ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma kwa urahisi, akisema benki hiyo sasa inahudumia zaidi ya wateja milioni 10, kupitia matawi zaidi ya 250, ATM zaidi ya 750 na mawakala zaidi ya 80,000.

Alisema mamilioni ya wateja pia wanatumia huduma za kidijitali, ikiwamo NMB Mkononi, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania, bila kujali anaishi au anafanya kazi wapi, anapata huduma za kifedha zilizo salama, za kuaminika na zinazopatikana kwa urahisi,” alisema.

Kulwa alisema NMB imeweka mkakati wa miaka mitano unaojulikana kama Ajenda 23, unaolenga kuoanisha ukuaji wa benki hiyo na maeneo yenye umuhimu katika maendeleo ya taifa.

Alisema kupitia mkakati huo, NMB imejielekeza katika sekta mbalimbali zenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa kwa wananchi.

Sekta hizo ni pamoja na kilimo, utalii, madini, uzalishaji viwandani, ujenzi na majengo, uchumi wa buluu, michezo, sekta ya ubunifu, fedha, usafirishaji na ugavi, TEHAMA, afya na elimu.

Alisema uwekezaji wa kifedha katika maeneo hayo ni sehemu ya juhudi za kuchochea uzalishaji, kukuza biashara na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

NMB YAIUNGA MKONO SERIKALI

Aidha, Kulwa aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji Tanzania, akisema jukwaa hilo limekuwa muhimu katika kuwakutanisha Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za kitaaluma na wadau wengine kujadili matumizi ya ushahidi katika kufanya maamuzi ya maendeleo.

Alisema NMB itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo, ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji Tanzania na tutaendelea kushirikiana katika safari ya maendeleo ya taifa letu,” alisema.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم