Breaking🔥

MLINZI AMTWANGA RISASI YA SHINGO DEREVA AKITOKA MSIKITINI NA KUFA,NI BAADA YA KUMNYIMA.SH, ELFU 15

DEREVA APIGWA RISASI, AUAWA KITUO CHA MAFUTA MOROGORO

Na Joseph Ngilisho | Morogoro

HALI ya taharuki imeibuka katika kituo cha mafuta kilichopo Kihonda Viwandani, Manispaa ya Morogoro, baada ya dereva wa lori, Feisal Jabir, mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 35 na 40,  kupigwa risasi na kuuawa na mlinzi wa kituo hicho.

Tukio hilo limetokea Septemba 9, 2026, ambapo marehemu alidaiwa kufika katika kituo hicho akiwa na lori na kulipaki kabla ya kuelekea msikitini.

Kwa mujibu wa mashuhuda, akiwemo Bakara Hussein, baada ya Feisal kurejea kutoka msikitini, kulitokea malumbano kati yake na mlinzi wa kituo hicho, ambaye baadaye anadaiwa kufyatua risasi iliyompiga dereva huyo akiwa ndani ya gari.

Mashuhuda hao wamedai kuwa tukio hilo lilisababisha hofu na taharuki miongoni mwa watu waliokuwa katika eneo hilo, huku marehemu akipoteza maisha kutokana na jeraha alilolipata.

Kaimu Afisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Scolastica Ndunga, amethibitisha kupokelewa kwa mwili wa marehemu katika hospitali hiyo.

Ndunga amesema mwili huo ulikuwa na jeraha shingoni.

Hata hivyo, chanzo rasmi cha malumbano hayo, mazingira halisi ya tukio na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mlinzi anayedaiwa kuhusika bado hazijaelezwa wazi na mamlaka.

Uchunguzi wa vyombo vya usalama unatarajiwa kubaini kilichotokea kabla na wakati wa tukio hilo, pamoja na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم