Ad
Breaking🔥

MKONGE WAGEUKA FURSA MPYA KWA WAKULIMA, VIWANDA VYAKABIDHIWA AMCOS.

 MKONGE WAGEUKA FURSA MPYA KWA WAKULIMA, VIWANDA VYAKABIDHIWA AMCOS.

Na Hadija Bagasha Tanga, 

Wakulima wadogo wa zao la mkonge mkoani Tanga wanatarajiwa kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao baada ya vyama vyao vya ushirika (AMCOS) kuanza kukabidhiwa viwanda vidogo vya kuchakata mkonge, hatua inayobadili mfumo wa huduma za uchakataji wa zao hilo katika ngazi ya mkulima.


Hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa mashine za kutosha za kuchakata mkonge, hali iliyokuwa ikisababisha sehemu ya zao hilo kukauka baada ya kuvunwa kabla ya kufikishwa kwenye hatua ya uchakataji na hatimaye sokoni.


Makabidhiano hayo yamefanyika katika hatua ya awali kati ya Bodi ya Zao la Mkonge Tanzania (TSB) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), huku AMCOS zikipewa nafasi ya kuendesha shughuli za uchakataji chini ya usimamizi wa TSB.


Hatua hiyo inafuatia maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 29, 2025, kuhusu kuwapatia wakulima mashine ili waweze kuendesha wenyewe shughuli za uchakataji wa mkonge.


Mwenyekiti wa wenyeviti wa AMCOS tano za zao la mkonge Wilaya ya Korogwe, Shadrack Lugendo, amesema kukabidhiwa kwa viwanda hivyo kunaweza kuondoa kikwazo kilichokuwa kikidhoofisha uzalishaji wa wakulima wadogo, hususan changamoto ya kuchelewa kuchakata zao baada ya kuvuna.


Amesema awali baadhi ya wakulima walilazimika kusubiri huduma za uchakataji kutokana na uhaba wa mashine, jambo lililosababisha mkonge kukauka na kuwaathiri kiuchumi.


“Tunaaahidi uzalishaji utakuwa mkubwa zaidi na ile mikonge ya wakulima ambayo ilikuwa inakauka kwa sababu ya huduma za uchakataji tutaikamilisha kwa sababu Bodi ya Mkonge inaendelea kuweka viwanda zaidi,” amesema Lugendo.


Kwa mujibu wa Lugendo, mfumo mpya unatoa fursa kwa mkulima kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa uzalishaji na uchakataji, badala ya kutegemea zaidi huduma kutoka kwa waendeshaji wengine.


“Matumaini yetu sasa ni kwamba uzalishaji utakuwa sehemu moja na ili uzalishaji uwe mzuri zaidi inatakiwa mwenye shamba ndiye aendeshe hizo Korona,” amesema.


Amesema hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wakulima wadogo huku akieleza kuwa AMCOS mbili za Magoma na Magunga tayari zimeanza kupata mikopo kwa ajili ya kuboresha uzalishaji na ununuzi wa mashine za kuchakata mkonge.


NSSF YAKABIDHI, AMCOS KUCHAKATA


Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saddy Kambona, amesema kukabidhiwa kwa viwanda hivyo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za zao la mkonge na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.


Amesema AMCOS zinapaswa kuwa na usimamizi madhubuti wa viwanda hivyo pamoja na kuhakikisha wakulima wadogo wanapata huduma kwa wakati ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na manufaa yanayotokana na zao hilo.


“Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma pale ambapo walikuwa wakifanya wenzetu wa SISALANA,  AMCOS waongeze jitihada, lengo la Serikali ni kuleta tabasamu kwa wakulima wadogo na Watanzania na tunaona kwa hatua hii tuna imani kwamba AMCOS zina nguvu kazi ya kutosha, kikubwa ni usimamizi na kufanya kwa ubora zaidi,” amesema Kambona.


Kambona amesema zao la mkonge linaendelea kuwa miongoni mwa mazao yenye nafasi katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na nyuzi pamoja na uwepo wa soko la kimataifa.


Amesema uwekezaji unaoendelea katika zao hilo unalenga pia kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu.


SISALANA YAONDOKA, AMCOS ZAPEWA JUKUMU. 


Kwa upande wake, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF katika makubaliano hayo, Ibrahimu Maftaa amesema makubaliano yaliyosainiwa ni hatua ya awali kuelekea kukamilisha mkataba utakaowapa AMCOS chini ya TSB mamlaka ya kuendesha mashine na shughuli za uchakataji wa mkonge.


Amesema awali baadhi ya shughuli hizo zilikuwa zikitekelezwa na SISALANA, kampuni tanzu ya NSSF, lakini sasa mfumo unaelekea kuwapa AMCOS nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika uendeshaji wa shughuli hizo.


“Tumeweza kusaini makubaliano ya awali kuweza kuendesha shughuli za mkonge ambazo zilikuwa zikiendeshwa na SISALANA, ambayo ni kampuni tanzu ya NSSF, na sasa tumewakabidhi TSB na AMCOS ambao wataweza kuendesha shughuli zote tulizokuwa tunazifanya,” amesema Maftaa.


Amesema taratibu nyingine zinaendelea kukamilishwa kabla ya kusainiwa kwa mkataba rasmi utakaoweka wazi mamlaka na majukumu ya AMCOS katika uendeshaji wa viwanda hivyo.


CHANGAMOTO MPYA: USIMAMIZI WA VIWANDA. 


Pamoja na kukabidhiwa kwa viwanda hivyo, utekelezaji wake unafungua hatua nyingine muhimu kwa AMCOS, ambayo ni kuhakikisha mashine zinatumika kwa ufanisi, zinatunzwa na huduma za uchakataji zinawafikia wakulima kwa wakati.


Kwa wakulima wa mkonge, uwezo wa kuchakata zao karibu na mashamba unaweza kupunguza muda kati ya uvunaji na uchakataji, kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa thamani wa zao hilo.


Hivyo, mafanikio ya mpango huo yatategemea siyo tu upatikanaji wa mashine, bali pia uwezo wa AMCOS kusimamia viwanda, kuwahudumia wakulima kwa wakati, kutunza mitambo na kuhakikisha uzalishaji unaendelea kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya soko.


Hatua hiyo sasa inaweka jukumu kubwa kwa wakulima kupitia AMCOS kutumia miundombinu hiyo kuongeza uzalishaji na kuifanya Tanga kuendelea kuwa kitovu muhimu cha zao la mkonge nchini.


Mwisho.

Post a Comment

أحدث أقدم