Ad
Breaking🔥

LUKUMAY AFADHILI MAFUNZO YA MADEREVA BODABODA NA DALADALA KUPUNGUZA AJALI NDURUMA,AWATAKA KUZINGATIA SHERIA,NA KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA

LUKUMAY AFADHILI,AZINDUA MAFUNZO YA BODABODA NA DALADALA  KUPUNGUZA AJALI NDURUMA,AWATAKA KUZINGATIA SHERIA

 Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

 
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amefadhili mafunzo ya madereva wa bodaboda na daladala katika Kata ya Nduruma, akisema elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za kupunguza ajali, majeraha na vifo barabarani.

Dkt. Lukumay alisema hayo Septemba 28,2026 katika kijiji cha Samalia-Nduruma wakati akifungua mafunzo hayo, akiwataka madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda maisha yao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.


Alisema takwimu za ajali za bodaboda zinaonyesha umuhimu wa kutoa elimu endelevu kwa madereva, akieleza kuwa mwaka 2024 kulikuwa na ajali 20 zilizohusisha vifo vya watu 19 na majeruhi 18.

Alisema mwaka 2025 ajali hizo ziliongezeka hadi 24, zilizosababisha vifo vya watu 15 na majeruhi 18, huku mwaka 2026 zikiwa saba, zilizosababisha vifo vya watu sita na majeruhi watatu.

“Lengo langu kubwa ni kuhakikisha mnafanya kazi zenu kwa ufanisi na usalama wa hali ya juu kwa ajili ya usalama wenu wenyewe na abiria mnaowabeba,” alisema Dkt. Lukumay.

Alisema ameamua kuunga mkono mafunzo hayo kutokana na nafasi kubwa ya bodaboda na daladala katika usafirishaji wa wananchi, akiwataka madereva kutumia maarifa watakayopata kubadili tabia na kuacha vitendo vinavyoweza kusababisha ajali.

Dkt. Lukumay pia aliwataka kuwa makini wanapoingia kwenye barabara kuu kutoka njia ndogo, akisisitiza kuwa maboresho ya miundombinu yanapaswa kwenda sambamba na nidhamu ya matumizi ya barabara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Arumeru (OCD), Beatrice Monga, aliwataka madereva kuifanya usalama kuwa jambo la kwanza, akisisitiza uzingatiaji wa sheria na matumizi sahihi ya vifaa vya kinga.

Monga pia aliwataka madereva kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na kushirikiana na polisi kutoa taarifa za watu wanaoshukiwa kujihusisha na uhalifu katika vituo vyao.

Diwani wa Nduruma, Samweli Laizer, aliwataka vijana kutumia elimu wanayopewa kuboresha maisha yao, akisema Serikali inaendelea kuweka fursa mbalimbali za kuwawezesha.

Wakati huo huo, wamiliki wa daladala Nduruma wamemuomba Dkt. Lukumay kuwasaidia kukamilisha malipo ya Sh milioni 26 zilizobaki katika ununuzi wa gari aina ya Costal





Ombi hilo liliwasilishwa kupitia risala iliyosomwa na Katibu wa Kikundi cha Daladala Nduruma, Amon Seguran, ambaye alisema kikundi hicho chenye zaidi ya wanachama 15 kimeanza uwekezaji wa pamoja katika usafirishaji.

Aidha, wazee wa koo za mila wa Kanda ya Olokye, Nduruma, walimpongeza Dkt. Lukumay kwa kuwa karibu na wananchi na kumkabidhi ombi la kusaidia ujenzi wa ukumbi wa wazee wa koo za mila katika eneo lililotengwa na Serikali katika Kijiji cha Samaria.

Walisema ukumbi huo utatumika kuhifadhi mila, desturi na historia ya jamii, pamoja na kutoa ushauri kwa vijana na kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii.






Ends


Post a Comment

أحدث أقدم