MGOMO WA MADEREVA WATINGISHA USAFIRI NCHINI
POLISI YAONYA WANAOWAZUIA MADEREVA, YASEMA MFUMO WA POINTI BADO HAJAANZA KUTUMIKA
Na ArushaDigital
Mgomo huo umeathiri huduma za usafiri katika baadhi ya maeneo, huku abiria wakikwama vituoni na safari za mabasi kusuasua, wakati malalamiko ya madereva yakihusisha pia kukamatwa kwa magari na hatua dhidi ya leseni zao.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kueleza kuwa mfumo wa pointi kwa madereva uko katika hatua ya majaribio.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa Kamati Maalum ya Usafirishaji Tanzania, Zacharia Phares Joshua, alisema kusitishwa kwa huduma za usafirishaji kunatokana na malalamiko ya madereva kuhusu mfumo huo.
“Kwa sababu mfumo mpya unapoingia unaweza kuwa na matokeo chanya au hasi, kikubwa ni namna gani tunatatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha hazisababishi matatizo mengine,” alisema Joshua.
Wakati malalamiko hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi Tanzania limeonya watu au vikundi vinavyowazuia madereva wa mabasi na malori kuendelea na safari, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Jumanne, Septemba 29, 2026, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadh Juma, alisema kuzuia vyombo vya usafiri au kuwafanyia hujuma madereva ni kinyume cha sheria.
CP Awadh pia alitoa ufafanuzi muhimu kwamba mfumo wa pointi za leseni bado haujaanza kutumika, huku akiwataka madereva na wananchi kutopuuzia taarifa zisizo rasmi zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Kauli hiyo imekuja wakati huduma za usafiri zikisuasua katika baadhi ya mikoa, ambapo madereva katika vituo vya mabasi vya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam wameripotiwa kusitisha safari wakieleza malalamiko kuhusu kukamatwa kwa magari, kufungiwa leseni na masuala yanayohusishwa na mfumo wa pointi.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya abiria kukwama katika vituo vya mabasi, huku Jeshi la Polisi likisema linaendelea kufuatilia mwenendo wa tukio hilo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
#ArushaDigital-UPDATES

Post a Comment