Ad
Breaking🔥

IAA YANG’ARA USIMAMIZI WA FEDHA, YANYAKUA TUZO YA KWANZA NCHINI

IAA YANG’ARA USIMAMIZI WA FEDHA, YANYAKUA TUZO YA KWANZA NCHINI

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeandika historia mpya baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kitaifa katika kundi la taasisi za umma zisizo za kibiashara zinazofanya vizuri katika usimamizi na matumizi bora ya fedha.

IAA imejinyakulia tuzo hiyo katika kipengele cha Best Financial Management Performance – Non-Commercial Entities, ikiwa ni kutambuliwa kwa utendaji wake katika usimamizi, ukusanyaji na matumizi ya fedha za umma kwa ufanisi na uwajibikaji.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la IAA, Dkt Mwamini Tulli, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratias Ndejembi, wakati wa kikao cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum), kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkuu wa IAA, Prof Eliaman Sedoyeka, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa mikakati ya chuo katika kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya fedha, kufuatia maelekezo ya Serikali ya kutaka taasisi za umma kuongeza ufanisi na kujisimamia kwa weledi.

Amesema IAA ilianza kuchukua hatua za makusudi katika kuboresha mifumo yake ya kifedha na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana zinatumika kwa ufanisi, hatua ambayo sasa imezaa matokeo na kuiwezesha taasisi hiyo kutambuliwa kitaifa.

“Baada ya maelekezo ya Serikali kuhusu taasisi za umma kujipambanua katika ukusanyaji na matumizi bora ya fedha, tulianza kufanya jitihada za dhati kuhakikisha tunatimiza azma hiyo. Leo tunajivunia kuona juhudi hizo zimetambuliwa,” amesema Dkt Sedoyeka.

IAA YAENDELEA NA AJENDA YA AJIRA

Prof. Sedoyeka amesema pamoja na mafanikio katika usimamizi wa fedha, IAA imeanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais kuhusu umuhimu wa taasisi za elimu kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaowawezesha kuajiriwa na kujiajiri.

Amesema chuo hicho kimeanza kuboresha mitaala yake ili iendane na mahitaji halisi ya soko la ajira na biashara, kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi na ushindani unaoongezeka.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Chuo, maboresho hayo yanahusisha maeneo mbalimbali ikiwamo fedha, utawala, bima, utalii, uanagenzi pamoja na huduma za posta na vifurushi, yakilenga kuwapa wanafunzi ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja katika soko la ajira na ujasiriamali.

VIJANA WANZISHA MAKAMPUNI

Prof. Sedoyeka amesema IAA pia imeweka mkazo katika kuwajengea vijana uwezo wa kubadili maarifa wanayopata darasani kuwa fursa za kiuchumi.

Amesema chuo kimeandaa wataalamu wanaowasaidia vijana kutambua na kuendeleza mawazo ya kibiashara, huku baadhi yao wakifanikiwa kuanzisha kampuni na biashara zao.

“Mpaka sasa tumefanikiwa kuwasaidia vijana kuanzisha kampuni 20, huku zaidi ya biashara 50 zisizo rasmi nazo zikiwa zimeanzishwa,” amesema.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa jukumu la IAA halijabaki kwenye kutoa elimu pekee, bali limepanuka hadi katika kuwawezesha vijana kutumia elimu na ujuzi wanaoupata kujenga ajira zao na kuchangia uchumi wa Taifa.

Mafanikio hayo, amesema, yanaendelea kuipa IAA msukumo wa kuwekeza zaidi katika ubora wa elimu, usimamizi wa rasilimali na programu zinazolenga kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na biashara.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post