Ad
Breaking🔥

KASEKENYE ATOA ONYO ZITO ARUSHA KABLA YA EL NIÑO,AITAKA TANROADS NA WANANCHI KUJIANDAA.

KASEKENYE ATOA ONYO ZITO ARUSHA KABLA YA EL NIÑO

....Aitaka TANROADS na wananchi kujiandaa, asisitiza mikondo ya maji isizuiwe

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenye, ametoa tahadhari kwa wananchi na viongozi wa Serikali za Mitaa jijini Arusha kuepuka kuzuia au kubadili mikondo ya asili ya maji, akisema hatua hiyo inaweza kusababisha mafuriko, kukatika kwa barabara na kuleta madhara makubwa kwa miundombinu na shughuli za wananchi.

Kasekenye alitoa kauli hiyo Septemba 28,2026 wakati akikagua ujenzi na maboresho ya miundombinu ya barabara jijini Arusha, inayotekelezwa na Serikali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Michuano ya AFCON, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa salama dhidi ya athari za mvua kubwa zinazoweza kujitokeza.

Alisema Serikali imeendelea kufanya maandalizi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo kukagua madaraja, kusafisha mifereji na kuhakikisha maeneo yanayoweza kuathiriwa na maji yanachukuliwa hatua mapema.

“Unapozuia maji kwenye mkondo unahatarisha shughuli zote za Watanzania, siyo za kwako. Tunaomba wananchi tushirikiane na viongozi wetu, hasa watendaji wa kata na vijiji, kuhakikisha maji yanaelekezwa kwenye mikondo yake,” alisema.

Kasekenye alisema baadhi ya wananchi wanaweza kuamua kupeleka maji kwenye njia nyingine kwa lengo la kujikinga na madhara, lakini hatua hiyo inaweza kusababisha hasara kubwa kwa watu wengine, hasa pale maji yanapobadilisha mwelekeo na kuelekea kwenye barabara, madaraja au maeneo ya makazi.

“Unaweza kujilinda wewe mwenyewe kwa kupeleka maji upande mwingine, lakini ukaleta madhara mengi sana kwa watu wengine. Kwa hiyo ni muhimu kila mmoja kuona suala hili ni jukumu lake,” alisema.

Alisema kipindi hiki ni muhimu kwa wananchi kuanza kusafisha na kuchimba mifereji, pamoja na kuhakikisha maji yanaelekezwa kwenye mikondo yake ya asili ili kupunguza uwezekano wa mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

TANROADS YAWEKA AKIBA YA VIFAA

Kasekenye alisema TANROADS Kanda ya Kaskazini imeanza maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, ikiwamo kuweka akiba ya vifaa vya dharura ambavyo vinaweza kutumika pale miundombinu inapoharibika.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kuhakikisha kuwa pale daraja linapoanguka au barabara inapokatika, hatua za dharura zinaweza kuchukuliwa kwa haraka.

“Wenzetu wa TANROADS wameshachukua vifaa ambavyo tunategemea. Kama daraja likianguka leo, tayari tuna stock ya vifaa ambavyo vinaweza kupelekwa. Kama vinatakiwa vifaa vya chuma, tayari tunavyo,” alisema.

Alisema maandalizi hayo yamezingatia maeneo mbalimbali nchini, huku vituo vya vifaa vikiwekwa katika maeneo ambayo yanaweza kusaidia usafirishaji wa haraka pale maafa yanapotokea.

ARUSHA, KILIMANJARO NA MANYARA KUJIANDAA

Naibu Waziri huyo alisema tahadhari hiyo ni muhimu zaidi kwa mikoa inayotarajiwa kupata mvua nyingi, ikiwamo Arusha, Kilimanjaro na Manyara, pamoja na maeneo mengine ya Kanda ya Kaskazini.

Alisema Serikali kupitia mifumo yake ya kukabiliana na maafa, ikiwamo uratibu unaofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, imeendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga yatakayotokea.

“Lazima tujiandae kuwa tayari. Serikali ina mfuko wa maafa ambao unapopata changamoto kubwa ni lazima tukabiliane nayo. Miradi itaendelea, lakini kunapotokea changamoto ambayo ni ya maafa, Serikali tayari imejiandaa kukabiliana nayo,” alisema.

AFCON YAWEKA MSUKUMO

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Arusha, Kasekenye alisema Serikali inaendelea kusimamia miradi hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya jiji hilo, ikiwamo maandalizi ya AFCON, ambayo yanahitaji miundombinu bora na inayoweza kuhudumia ongezeko la shughuli na wageni.

Alisema pamoja na kasi ya kukamilisha miradi, Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa usanifu na utekelezaji wake unazingatia changamoto za maji, ili miundombinu inayojengwa iweze kuhimili mazingira halisi ya Arusha.

“Wakati tunasanifu na kutengeneza miradi hii, tunajua tunapokea maji mengi na suala hilo limezingatiwa kwenye usanifu. Lakini El Niño ni janga la asili ambalo wakati mwingine linaweza kuwa na nguvu zaidi ya matarajio,” alisema.

Kasekenye alisema maandalizi hayo yanapaswa kwenda sambamba na ushirikiano wa wananchi, wataalamu na viongozi wa Serikali za Mitaa, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu ya barabara si jukumu la Serikali pekee.

“Hii siyo kazi ya Serikali peke yake. Wananchi, viongozi wa kata na vijiji na wataalamu wote tunapaswa kushirikiana kuhakikisha mikondo ya maji inalindwa na miundombinu yetu inalindwa,” alisema.

Enda

Post a Comment

Previous Post Next Post