**Asema miradi ikamilike Desemba, ataka taasisi za maji, umeme na mawasiliano kuondoa vikwazo vya ujenzi
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Kasekenya alisema hayo leo Seotember 29,2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara mbalimbali jijini Arusha, zikiwamo zinazotekelezwa katika maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya usafiri jijini Arusha, si kwa ajili ya AFCON pekee, bali pia kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora zitakazotumika kwa miaka mingi baada ya mashindano hayo.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba hii miradi isikwame. Hii miradi ikamilike ndani ya muda. Kwa upande wetu, ndani ya muda ni Desemba mwaka huu,” alisema Kasekenya.
Alisema Tanzania, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, inaendelea na maandalizi ya AFCON, hivyo ni muhimu Arusha kuwa na miundombinu inayokidhi hadhi ya mashindano hayo ya kimataifa.
Kasekenya alisema Serikali haitaki uwekezaji unaofanyika kwa ajili ya AFCON uwe wa muda mfupi, bali unapaswa kuacha miundombinu itakayowanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Alisema barabara zinazojengwa zinajumuisha njia za magari, maeneo ya watembea kwa miguu pamoja na taa, hatua ambazo alisema zitasaidia kuufanya mji wa Arusha kuwa wa kisasa na wenye kuvutia.
“AFCON ni ya muda mfupi, lakini miundombinu yetu itaendelea kubaki na kuishi. Kwa hiyo tayari tunakuwa tumeufungua mji wa Arusha na kuupendezesha,” alisema.
Katika ziara hiyo, Kasekenya alizitaka taasisi zinazohusika na huduma za maji, umeme na mawasiliano kushirikiana kwa karibu na wakandarasi katika kuhamisha miundombinu inayokutana na maeneo ya ujenzi.
Alisema baadhi ya barabara zinapopanuliwa, wakandarasi hukutana na mabomba ya maji, nyaya za umeme na miundombinu ya mawasiliano iliyopo chini ya ardhi, hali inayoweza kuchelewesha kazi.
“Tunachotaka sisi ni muda tuliopanga ukamilike. Wasiwe wanasema maji au umeme ndiyo vimesababisha kuchelewa. Tunaomba wale wanaohusika wafanye kazi haraka,” alisema.
Alisema Serikali inatambua kuwa kuhamisha miundombinu hiyo kunaweza kuathiri huduma kwa wananchi kwa muda, lakini taasisi husika zinapaswa kuchukua hatua kwa haraka ili kuzuia miradi kuchelewa.
Kasekenya alisema usanifu wa barabara hizo umezingatia pia changamoto ya mafuriko ambayo imekuwa ikiikabili Arusha, hasa kutokana na jiografia ya mji huo na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema baadhi ya makaravati yanayojengwa yameongezwa uwezo mara kadhaa ikilinganishwa na yaliyokuwapo awali, ili kuruhusu maji mengi kupita wakati wa mvua kubwa.
“Tumeona kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi maji yamekuwa mengi. Kwa hiyo makaravati yameongezwa uwezo ili maji yaweze kupita,” alisema.
Alisema barabara hizo pia zinajengwa pamoja na mitaro mikubwa itakayosaidia kukusanya na kuelekeza maji kwenye maeneo sahihi, badala ya kuyaacha yakielekea kwenye makazi ya wananchi.
Kasekenya pia alieleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara yenye urefu wa takribani kilomita 18 kutoka Mianzini na Sambasha hadi Ngaremtoni, akisema mradi huo unalenga pia kudhibiti maji yanayotoka maeneo ya juu ya mji.
Katika hatua nyingine, Kasekenya alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wa barabara ya Tengeru–Mbuguni–Mererani hadi kuungana na KIA, akisema mradi huo utasaidia kuimarisha mtandao wa usafiri na kufungua maeneo mapya kwa shughuli za kiuchumi.
Alisema ongezeko la watu na shughuli za biashara jijini Arusha limeongeza mahitaji ya miundombinu bora ya usafiri.
Kasekenya aliwataka wananchi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, akisema ujenzi wa miundombinu mikubwa unaweza kuleta usumbufu wa muda, lakini manufaa yake yatakuwa ya muda mrefu.
Alisema Serikali inalenga kuona Arusha ikiwa na mtandao wa barabara unaoendana na hadhi yake kama mji muhimu wa utalii, biashara na mikutano ya kimataifa.
“Wananchi watoe ushirikiano. Tunachojenga sasa si kwa ajili ya AFCON pekee. Hizi barabara zitaendelea kutumika na wananchi wa Arusha kwa miaka mingi,” alisema Kasekenya.
Ends..


Post a Comment