LUKUMAY APOKELEWA KWA SHANGWE NDURUMA,MSAFARA WAKE WATIKISA , WANANCHI WAFURIKA WAMWAGIA KERO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Msafara wa mbunge huyo wenye zaidi ya magari 50, uliongozwa na waendesha bodaboda zaidi ya 100 waliokuwa wakifanya mbwembwe, madaga na madowido, huku wakipita katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Nduruma wakimsindikiza mbunge wao.
Wananchi waliokuwa pembezoni mwa barabara walijitokeza kumlaki Dkt Lukumay, huku baadhi wakipaza sauti za shangwe na wengine wakimweleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Katika ziara hiyo, Dkt Lukumay alitembelea Shule ya Sekondari Olemedeye na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la wasichana, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza usalama na ustawi wa wanafunzi.Hata hivyo, pamoja na mapokezi hayo, wananchi walitumia fursa hiyo kumwaga mbele ya mbunge huyo kero zinazowakabili, ikiwamo changamoto ya makorongo yanayosababisha mafuriko, hali inayodaiwa kuhatarisha maisha, kuharibu nyumba na kukwamisha usafiri wakati wa mvua.
Alisema katika msimu uliopita wa mvua, maji hayo yaliingia kijijini na kuangusha nyumba kadhaa, huku akieleza hofu kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi endapo mvua kubwa zitanyesha.
“Korongo limeacha njia yake na kufuata makazi ya watu. Msimu uliopita maji yaliingia kijijini na kuangusha zaidi ya nyumba tatu au nne. Tunaomba Mheshimiwa Mbunge alibebe suala hili kwa uzito,” alisema Jeremia.
Aidha, wananchi walieleza changamoto ya barabara inayounganisha Majimoto na maeneo mengine ya Nduruma, Karangai na mjini Arusha, wakisema wakati wa mvua baadhi ya maeneo hukatika kabisa kutokana na maji na makorongo.
Jeremia alisema hali hiyo imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi, ikiwamo usafirishaji wa mazao na wananchi wanaokwenda kutafuta huduma muhimu.
Kwa upande wake, Baraka Filipo, mkazi wa Nduruma, alisema wakazi wanaotumia barabara kuelekea Mnada wa Loki hukumbana na changamoto kubwa wakati wa mvua kutokana na uwepo wa makorongo.
Alisema mnada huo ni muhimu kwa shughuli za wananchi, lakini mazingira yake bado yanahitaji kuboreshwa, hasa upatikanaji wa maji na huduma za vyoo.
Filipo, ambaye ni mwendesha bodaboda, pia aliiomba Serikali kuboresha barabara kwa kuzingatia mwelekeo wa maji wakati wa ujenzi na matengenezo ili miundombinu hiyo isiharibiwe kila msimu wa mvua.
Mbali na barabara na makorongo, wananchi walieleza changamoto ya kivuko cha Mto Maroroi, wakisema wakati wa mvua maji yanapoongezeka, wananchi, hasa wajawazito na wagonjwa, hupata wakati mgumu kuvuka kwenda kupata huduma.
Walisema changamoto hiyo imekuwa ikijirudia kila mwaka na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, huku wakitaka hatua za kudumu zichukuliwe badala ya kusubiri maji yapungue kila mvua inaponyesha.
Wananchi pia waliwasilisha kero ya upatikanaji wa umeme katika Kitongoji cha Zaire, wakisema licha ya baadhi ya maeneo kupata huduma hiyo, bado idadi kubwa ya wakazi hawajafikiwa.
Aidha, walitaja hitaji la urasimishaji wa mashamba yao ili waweze kupata hati na kutumia ardhi hiyo kama dhamana katika shughuli za maendeleo na kilimo.
LUKUMAY ATOA KAULI
Akizungumza baada ya kusikiliza kero hizo, Dkt Lukumay alisema ziara yake imelenga kusikiliza wananchi moja kwa moja na kubaini changamoto zinazohitaji hatua za haraka katika Jimbo la Arumeru Magharibi.Alisema suala la miundombinu, hususan barabara, makorongo na vivuko, haliwezi kutenganishwa na usalama wa wananchi na maendeleo ya shughuli zao za kiuchumi.
Dkt Lukumay aliwahakikishia wananchi kuwa kero hizo atazifikisha katika mamlaka husika na kuzifuatilia ili hatua zichukuliwe kwa kuzingatia uhitaji na mazingira halisi ya maeneo hayo.
Akizungumzia changamoto ya mvua, alisisitiza umuhimu wa wataalamu wa halmashauri kutoka ofisini na kufika maeneo yenye changamoto ili kuona hali halisi na kupanga hatua zinazofaa kukabiliana na mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Alisema pia atafuatilia changamoto ya kivuko cha Mto Maroroi pamoja na barabara zinazounganisha vijiji vya Kata ya Nduruma, akisisitiza kuwa miundombinu hiyo ni muhimu kwa wananchi kufikia huduma za kijamii na masoko.
Kwa upande wa elimu, Dkt Lukumay alisema ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Olemedeye ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Ziara hiyo iliendelea katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Nduruma, huku wananchi wakitumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa mbunge huyo na kuomba ziwe sehemu ya vipaumbele vya maendeleo vya jimbo.
Ends



















إرسال تعليق