LUKUMAY AFANIKISHA HARAMBEE YA MILIONI 31.1
......AWAASA VIONGOZI WA DINI KUOMBEA AMANI, RAIS SAMIA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Katika harambee hiyo, iliyolenga kuchangisha Sh milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uimbaji, Dkt. Lukumay mwenyewe alichangia Sh milioni tatu, huku akiwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa ili amani, upendo na utulivu viendelee kudumu.Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia Kwaya ya Mwangaza kuboresha vifaa vya uimbaji na kuongeza ufanisi katika huduma ya muziki wa kanisani.
“Tumepata milioni tatu. Hii ni kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu. Natoa shukrani kubwa kwa Askofu kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika kanisa lako,” alisema.
Alisema licha ya kuwa na majukumu mengi yanayohitaji fedha, aliamua kutenga sehemu ya alichopata kwa ajili ya kusaidia kazi ya Mungu na shughuli za maendeleo.
“Muziki ni sehemu ya ibada. Kwaya inafanya kazi kubwa katika kulitumikia Kanisa, kwa hiyo ni muhimu waumini na wadau kuendelea kuiunga mkono,” alisema.
Dkt. Lukumay aliwataka waumini na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia ili kufikia Sh milioni 100 zilizowekwa kama lengo la harambee hiyo.
AWAASA VIONGOZI WA DINI KUOMBEA AMANI
Alisema amani ni msingi wa shughuli za maendeleo na ustawi wa wananchi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuilinda na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
“Askofu, tuendelee kuombea amani nchini, tuwe na upendo na furaha katika nchi yetu, iendelee kuwa na utulivu,” alisema.
Pia aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuiombea Serikali pamoja na viongozi wa nchi, akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tuendelee pia kuombea Serikali yetu ya Awamu ya Sita na viongozi wetu na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumuombe aendelee kuwa na afya njema na atuongoze vizuri ili aweze kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema.
‘KAZI YANGU NI KUSIKILIZA WANANCHI’
Dkt. Lukumay alisema moja ya majukumu yake makubwa kama mbunge ni kusikiliza changamoto za wananchi na kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi nyingine kuzitafutia ufumbuzi.
Aliwataka wananchi kutokuwa kimya wanapokabiliwa na changamoto, bali kuzifikisha kwa viongozi wao ili hatua ziweze kuchukuliwa.
“Mimi sasa hivi sina kazi nyingine ni kusema tu. Mtu yeyote mwenye shida yake aniambie. Mimi ndiyo kazi yangu,” alisema.
Alitoa mfano wa mwananchi mmoja kutoka kata ya mbali aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo na kufikia hatua ya kutaka kuuza nyumba yake ili kupata fedha za matibabu.
Alisema baada ya kufikishiwa suala hilo, alilifanyia kazi na mwananchi huyo akaweza kupata matibabu bila kulazimika kuuza nyumba yake.
“Anatoka kata ya mbali, ana ugonjwa wa figo mpaka anataka kuuza nyumba. Nimeuchukua, sasa hivi anatibiwa bure kwa sababu Serikali yetu imeweza kufanya suluhisho,” alisema.
Alisema mfano huo unaonyesha umuhimu wa wananchi kushirikiana na viongozi wao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
‘HATUNA NCHI NYINGINE’
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Lukumay aliwataka Watanzania kuendelea kuilinda Tanzania, kudumisha umoja na mshikamano na kushirikiana katika shughuli za maendeleo.
“Hatuna nchi nyingine tunayojua, tuna nchi ya Tanzania. Tuendelee kuombea amani na tushirikiane tufanye,” alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji Loshilye Mollel alisema Kanisa limeridhishwa na utendaji wa Dkt. Lukumay katika kuwahudumia wananchi wa Arumeru Magharibi.Alisema Kanisa litaendelea kumuombea mbunge huyo na kumuunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Tutaendelea kukuombea usiku na mchana kwa sababu tunaona namna unavyowatumikia wananchi,” alisema.
Katika harambee hiyo, viongozi wa Kanisa pia walitoa maombi mazito kwa Dkt. Lukumay, wakimtaka aendelee kulitumikia jimbo hilo kwa uadilifu, akimtanguliza Mungu katika uongozi wake.
Harambee hiyo ni sehemu ya mpango wa Kwaya ya Mwangaza kukusanya Sh milioni 100 kwa ajili ya kununua na kuboresha vifaa vya uimbaji vitakavyosaidia kuongeza ufanisi wa huduma ya muziki katika ibada.
Ends











إرسال تعليق