DC KARANGA AKANUSHA KUAMURU KUFYEKWA KWA MAZAO HEKARI 27, UCHOMAJI WA NYUMBA OLDEANI
Na Joseph Ngilisho | KARATU
MKUU wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, amekanusha madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba alihusika au alitoa amri ya kufyekwa kwa Hekari 27 za mazao ya wananchi katika eneo lenye mgogoro la Kijiji cha Oldeani, Kata ya Endabash, wilayani Karatu.DC Karanga akiongea kwa simu na mwandhi wa Habari amesema ofisi yake haikutoa agizo la kufyekwa kwa migomba, miwa, mahindi wala mazao mengine yaliyokuwa yakilimwa na wananchi katika eneo hilo, akieleza kuwa taarifa za tukio hilo aliziona kupitia mitandao ya kijamii.
Amesema madai yanayomhusisha moja kwa moja na uharibifu wa mazao na mali za wananchi hayana ukweli, akisisitiza kuwa yeye binafsi hakutoa maelekezo ya kutekelezwa kwa hatua hizo.
“Ofisi yangu haikutoa agizo la kufyeka mazao hayo. Mimi mwenyewe niliona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii,” amesema Dkt. Karanga.
MGOGORO WA TANGU 2017
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mgogoro wa eneo hilo si wa hivi karibuni, bali umechukua miaka kadhaa tangu mwaka 2017, kipindi ambacho yeye hakuwa bado Mkuu wa Wilaya ya Karatu.
Amesema tangu kuanza kwa mgogoro huo, wananchi waliokuwa wakiishi au kutumia eneo hilo wamekuwa wakielekezwa mara kadhaa kuliondoa, kwa madai kwamba eneo hilo linamilikiwa na mwekezaji wa Kongoni Estate.
Amesema katika hatua mbalimbali za kushughulikia mgogoro huo, viongozi wa wilaya pamoja na wataalamu wa kilimo waliwahi kufika katika eneo hilo na kutoa maelekezo kwa wananchi kuondoka.
Dkt. Karanga amesema miongoni mwa hoja zilizokuwepo ni matumizi ya eneo hilo na masuala yanayohusiana na vyanzo vya maji.
Amesema baada ya hatua mbalimbali za kiutawala kushindikana kumaliza mgogoro huo, mwekezaji aliamua kufikisha suala hilo mahakamani.
Kwa mujibu wa Dkt. Karanga, wananchi walipatiwa notisi za kuondoka kupitia court broker, hatua ambayo aliieleza kuwa ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa kisheria uliokuwa umefanyika.
Hata hivyo, amesema yeye alipoingia katika suala hilo alikutana na pande zote mbili na kusisitiza umuhimu wa wananchi kupewa muda wa kutosha ili waweze kuondoka kwa amani badala ya kuchukuliwa hatua kwa nguvu.
“Nilipokutana na pande zote, msisitizo wangu ulikuwa wananchi wapewe muda wa kutosha ili waondoke kwa amani,” amesema.
AKANUSHA TUHUMA ZA VIBOKO, LOCKUP
Mbali na madai ya kuamuru kufyekwa kwa mazao, Dkt. Karanga pia amekanusha tuhuma nyingine nzito zinazomhusisha na kukamatwa kwa wananchi waliokuwa wakilalamikia eneo hilo.
Baadhi ya wananchi hao wamekuwa wakidai kupitia mitandao ya kijamii kwamba waliwekwa lokapu na kwamba walikuwa wakipigwa viboko vitatu kila asubuhi kwa maagizo ya Mkuu huyo wa Wilaya.
Dkt. Karanga ameyakana madai hayo, akisema ofisi yake haikutoa amri hiyo na wala Jeshi la Polisi halikuhusika na tukio hilo kwa maelekezo yake.
Amesema madai hayo yamekuwa yakisambazwa bila yeye kuhusishwa katika tukio hilo na kuwataka wananchi na wadau wengine kutumia taratibu za kisheria pale wanapokuwa na malalamiko.
WANANCHI WADAI MAZAO, NYUMBA VIMEHARIBIWA
Awali, wakazi watatu wa eneo hilo waliosikika kupitia mitandao ya kijamii walimtuhumu Dkt. Karanga kwa kuhusika na agizo la kufyekwa kwa mazao yao katika eneo lenye ukubwa wa takribani hekari 27.
Wananchi hao walidai kuwa mazao yaliyoharibiwa yalikuwa yakijumuisha migomba, miwa na mahindi, huku wakidai pia kuwa nyumba zao zilichomwa moto wakati wa zoezi hilo.
Aidha, mmoja wa walalamikaji alidai kuwa kiasi cha Sh5 milioni kilichokuwa ndani ya nyumba yake kilipotea, pamoja na vitu vingine vya thamani vya ndani ya nyumba.
Walalamikaji hao pia walieleza kuwa uharibifu wa mazao umeathiri maisha yao kwa kuwa mazao hayo yalikuwa sehemu ya chakula na kipato cha familia zao.
Hata hivyo, madai hayo ni ya wananchi waliosikika kupitia mitandao ya kijamii na yamekanushwa na Mkuu wa Wilaya, ambaye amesema ofisi yake haikutoa amri ya kufanyika kwa uharibifu huo.
DC: HESHIMUNI UMILIKI WA ARDHI
Dkt. Karanga amewataka wananchi kuheshimu maeneo yanayomilikiwa na watu wengine na kuacha tabia ya kuingia au kutumia maeneo bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema migogoro ya ardhi inapaswa kushughulikiwa kwa kutumia mamlaka na vyombo vinavyotambulika kisheria, badala ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Pia amewataka wananchi wanaohusika katika migogoro ya ardhi kufuata maamuzi na taratibu zinazotolewa na vyombo vya sheria.
AWATAKA WAANDISHI KUSIKILIZA PANDE ZOTE
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuripoti taarifa zinazohusu migogoro ya ardhi, akisisitiza umuhimu wa kusikiliza pande zote zinazohusika.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuhakikisha taarifa zinazofikishwa kwa umma zinakuwa na usawa na zinazingatia ukweli wa kila upande.
Kauli hiyo imekuja wakati mgogoro wa eneo la Oldeani ukiendelea kuzua mjadala, huku wananchi wakitoa madai mbalimbali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika eneo hilo na Serikali ya Wilaya ikisisitiza kuwa suala hilo lina historia ya muda mrefu na limewahi kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Ends..
إرسال تعليق