Ad
Breaking🔥

WMA YAZINDUA MKAKATI MPYA, YAPIGA VITA UDANGANYIFU,SERIKALI YATOAMAAGIZO MAZITO

WMA YAZINDUA MKAKATI MPYA, YAPIGA VITA UDANGANYIFU,SERIKALI YATOAMAAGIZO MAZITO 

....Vipimo milioni 5.5 vyahakikiwa ndani ya miaka mitano, WMA yazindua mkakati mpya wa miaka mitano, Serikali yataka uadilifu kulinda uchumi na Dira ya Taifa 2050.

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SERIKALI imewataka watumishi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kusimamia kwa uadilifu ukaguzi wa vipimo nchini na kutokubali vitendo vya udanganyifu vinavyohatarisha ubora wa bidhaa, huku ikisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa vipimo ni nguzo muhimu ya kujenga uchumi wenye ushindani na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Onyo hilo limetolewa wakati Wakala wa Vipimo ukizindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa 2026/27 hadi 2030/31, utakaokuwa dira ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi kijacho, ukilenga kuongeza matumizi ya teknolojia, kuboresha utoaji huduma na kuimarisha utawala bora katika sekta ya vipimo.

Akifungua Kikao cha 38 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo jijini Arusha leo Jumapili,Agosti 02,2026 kilichowakutanisha wajumbe 77 kutoka maeneo mbalimbali nchini, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema WMA imeendelea kuwa mhimili muhimu wa kulinda uchumi wa taifa kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wakala huo umehakiki zaidi ya vipimo milioni 5.5 nchini, hatua ambayo imeimarisha ulinzi wa walaji, kuongeza uwazi katika biashara na kujenga mazingira bora ya ushindani.

Kwa mujibu wa Londo, serikali imepanua huduma za WMA kwa kufungua ofisi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ili kusogeza huduma karibu na wananchi na wafanyabiashara, hatua iliyorahisisha uhakiki wa vipimo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Alisisitiza kuwa ukuaji wa biashara unategemea uwepo wa imani kati ya mnunuzi na muuzaji, huku akieleza kuwa vipimo sahihi ndiyo msingi wa kujenga uaminifu huo, hasa katika kipindi hiki ambacho biashara nyingi zinafanyika kupitia mifumo ya kidijitali.

"Leo watu wanaagiza bidhaa kwa njia ya mtandao na wengine hulipia kabla hata mzigo haujawafikia. Imani hiyo inajengwa na uwepo wa mifumo madhubuti ya serikali, ikiwemo usimamizi wa vipimo sahihi," alisema.

Naibu Waziri huyo alionya kuwa udanganyifu wa vipimo husababisha hasara kwa walaji na wafanyabiashara, hupunguza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kudhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.

Aliwataka watumishi wa WMA kutokubali kushawishiwa au kuchezewa kwa vipimo kwa maslahi binafsi, akisema jukumu lao ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoingizwa kutoka nje zinazingatia viwango vinavyokubalika ili ziweze kushindana katika soko la kikanda na kimataifa.

"Kazi ya WMA ni ya kizalendo kwa kuwa inalinda uchumi wa taifa, huongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea uzalishaji wenye viwango na biashara yenye ushindani," alisema.

Katika kikao hicho, WMA pia ilizindua rasmi Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa 2026/27 hadi 2030/31, unaolenga kuimarisha utendaji wa taasisi, kuongeza matumizi ya teknolojia katika huduma za vipimo, kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Alban Kihulla, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, alisema taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini bado inakabiliwa na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuongeza ufanisi.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu wa watumishi, mahitaji ya kuendelea kuimarisha teknolojia ya vipimo, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya utoaji huduma.

Kihulla alisema mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano mzuri kati ya menejimenti na wafanyakazi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kupitia ongezeko la mishahara, maboresho ya posho na mazingira bora ya kazi.

Alisema Mpango Mkakati mpya umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na utawezesha taasisi kuongeza ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia na uwajibikaji, sambamba na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania kupitia mifumo bora ya vipimo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Modest Mkude, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, alisema serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo wilayani humo, hatua iliyoboa huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi.

Alisema fedha hizo zimeelekezwa katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu, ambapo zimewezesha ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali muhimu inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Arusha.







Ends.

Post a Comment

أحدث أقدم