TANZANIA YATOA MAONI MUSWADA WA BIDHAA ZA AFYA EAC,DKT LUKUMAY ASHIRIKI MASHAURIANO EALA.
Na Joseph Ngilisho | DODOMA
TANZANIA imeanza kutoa maoni yake kuhusu Muswada wa Sheria ya Bidhaa za Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Medical Products Bill, 2025), unaolenga kuweka mfumo wa pamoja wa udhibiti wa dawa na bidhaa za afya katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, leo Agosti 18, 2026, ameshiriki katika mashauriano ya Kamati ya Kudumu ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA Committee on General Purpose) yanayofanyika jijini Dodoma.
Mashauriano hayo ya siku mbili, yaliyoanza Agosti 17 na kuhitimishwa leo, yamewaleta pamoja wadau mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni ya Tanzania kuhusu muswada huo kabla ya hatua zinazofuata za mchakato wa kutunga sheria katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Muswada huo unalenga kuimarisha ushirikiano na kuoanisha mifumo ya udhibiti wa bidhaa za afya katika nchi wanachama wa EAC, hatua inayotarajiwa kuwa na mchango katika kuboresha upatikanaji wa dawa salama na zenye ubora kwa wananchi wa Jumuiya hiyo.
Miongoni mwa maeneo yanayolengwa na muswada huo ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, kuimarisha viwango vya ubora na usalama wa dawa, pamoja na kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa dawa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, muswada huo unalenga kuweka mifumo inayofanana katika usajili na udhibiti wa bidhaa za afya, huku ukisisitiza kuimarishwa kwa udhibiti dhidi ya dawa zisizo na ubora na bidhaa bandia zinazoweza kuhatarisha afya na usalama wa wananchi.
Ushiriki wa Tanzania katika mashauriano hayo unalenga kuhakikisha masuala muhimu kwa nchi yanazingatiwa katika mfumo wa kikanda, hususan katika kuhakikisha kuwa sheria itakayopitishwa inaleta uwiano kati ya ushirikiano wa kikanda na mahitaji halisi ya sekta ya afya ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Tanzania, ushirikiano huo pia unaweza kuwa muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya ndani ya Jumuiya, kupunguza changamoto za upatikanaji wa dawa na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora wa bidhaa zinazotumika katika huduma za afya.
Mashauriano hayo ni sehemu ya mchakato wa kupata maoni ya wadau kabla ya Muswada wa Sheria ya Bidhaa za Afya wa EAC, 2025, kuendelea na hatua nyingine za kisheria ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ends..

إرسال تعليق