TANGA YAGEUKA KITOVU CHA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU
Na Hadija Bagasha | TANGA
TANGA. Mkoa wa Tanga umegeuka kuwa kitovu cha elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu baada ya kuanza kwa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, huku Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akitarajiwa kuzindua rasmi maonyesho hayo leo, Agosti 18, 2026.
Maonyesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga, yamewakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya mafunzo na ufundi stadi pamoja na taasisi zinazojihusisha na sayansi, teknolojia na ubunifu.
Yalianza Agosti 15 na yanatarajiwa kuendelea hadi Agosti 24, yakilenga kuwaunganisha wananchi, wanafunzi, watafiti, wabunifu na wadau wa elimu ili kuonyesha kwa vitendo namna elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kuchochea maendeleo ya Taifa na kufanikisha Dira ya Taifa 2050.
BILIONI 156 ZATUMIKA ELIMU TANGA
Akizungumza kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, alisema Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio, huku usalama wa washiriki na wananchi ukipewa kipaumbele.
“Tanga inajivunia kuwa mwenyeji wa maonyesho haya. Tunawahakikishia Wizara ya Elimu na wananchi kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wote wa maonyesho,” alisema Dk. Batilda.
Alisema maonyesho hayo yana umuhimu mkubwa katika kuonyesha mchango wa elimu, ujuzi na ubunifu katika kujenga Tanzania inayolengwa kupitia Dira ya Taifa 2050.
Kwa mujibu wa Dk. Batilda, zaidi ya Sh156 bilioni zimeelekezwa katika kuboresha sekta ya elimu mkoani humo, hatua aliyoieleza kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kufundishia.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji unaofanyika katika sekta ya elimu, huku akiipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kuunga mkono maonyesho hayo.
VIJANA KUPATA FURSA
Dk. Batilda alisema maonyesho hayo hayalengi kuonyesha bunifu na teknolojia pekee, bali pia yameandaliwa kuwawezesha vijana kupata taarifa kuhusu fursa za elimu na mafunzo.
Alisema wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu watapata fursa ya kupata mwongozo kuhusu taratibu za maombi, fursa za masomo na masuala mbalimbali yanayohusiana na elimu ya juu.
“Vijana wanaoanza mchakato wa kujiunga na vyuo vikuu watapata fursa ya kuelekezwa namna sahihi ya kujaza maombi na kupata taarifa nyingine muhimu kuhusu elimu ya juu,” alisema.
Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 hauwezi kuwa jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushiriki wa taasisi za elimu, sekta binafsi, watafiti, wabunifu na wananchi.
Kaulimbiu ya maonyesho hayo ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa 2050.”
BUNIFU ZA KUTATUA CHANGAMOTO
Kwa upande wake, Flavian Sanga, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alisema chuo hicho kimewasilisha bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta ya afya.
Naye Shaphii Hamisi kutoka Chuo cha Uhandisi na Teknolojia cha Al-Maktoum alisema wamewasilisha bunifu zinazolenga kupunguza msongamano wa magari kwenye taa za barabarani, pamoja na mfumo wa kuuza maji katika vioski bila kuhitaji uwepo wa muuzaji.
Bunifu hizo, alisema, ni sehemu ya jitihada za kutumia maarifa na teknolojia kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi katika maisha ya kila siku.
MWIGULU KUFUNGA
Baada ya uzinduzi wa maonyesho hayo unaotarajiwa kufanywa leo na Profesa Mkenda, shughuli zitaendelea hadi Agosti 24, ambapo Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga.
Dk. Batilda amewataka wananchi wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Usagara kujionea bunifu, teknolojia, tafiti na fursa mbalimbali zinazotolewa na washiriki.
Alisema ushiriki wa wananchi ni muhimu kwa kuwa maonyesho hayo yanatoa fursa ya kujifunza, kubadilishana maarifa na kutambua hatua ambazo Tanzania imepiga katika elimu, utafiti, teknolojia na ubunifu.
Maonyesho hayo pia yanatarajiwa kuwa jukwaa la wabunifu kuonyesha kazi zao, kupata mrejesho, kubadilishana uzoefu na kutafuta fursa za kukuza bunifu zinazoweza kutatua changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Ends.




إرسال تعليق