MBUNGE WA MOSHI VIJIJINI AKATAA ANASA, AWEKEZA KWENYE BARABARA
Na Joseph Ngilisho
MOSHI. Mbunge wa Moshi Vijijini, Moris Makoi, amesema ameamua kujinyima baadhi ya starehe za uongozi, ikiwemo matumizi ya magari ya kifahari, na badala yake kuelekeza nguvu na rasilimali katika kutatua changamoto ya barabara inayowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Makoi amesema uamuzi huo unatokana na ahadi alizowapa wananchi wakati wa kampeni, akieleza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha jimbo linapata vifaa vya kutosha vya kuboresha miundombinu ya barabara.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibosho Magharibi katika mkutano wa kuwashukuru kwa kumpigia kura na kusikiliza changamoto zao, Makoi amesema ameamua kuchagua maendeleo ya wananchi badala ya kutumia fedha katika vitu vya kifahari.
“Nimekubali kukataa kuwa Hesau. Hesau aliuza uko kwa sababu ya tamaa ya chakula. Mimi nimeshinda hiyo tamaa ya magari ya kifahari ili tuweze kutengeneza barabara kwa pamoja,” amesema.
Amesema uamuzi huo umeenda sambamba na upatikanaji wa grader mpya, ambayo inalenga kuongeza kasi ya ukarabati na uboreshaji wa barabara za vijijini katika Jimbo la Moshi Vijijini.
Kwa mujibu wa Makoi, kwa sasa jimbo lina grader mbili, ambapo moja ipo maeneo ya Vunjo na nyingine imeelekezwa Kibosho Magharibi, ambako alitarajia kuanza kazi ya kusafisha na kuboresha barabara mara baada ya mkutano huo.
Makoi amesema lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanaona matokeo ya uongozi wake kupitia utekelezaji wa miradi inayogusa maisha yao moja kwa moja, akisisitiza kuwa nafasi ya ubunge ni dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Amesema ataendelea kuweka mbele mahitaji ya wananchi na kutumia rasilimali zinazopatikana katika kutatua changamoto zinazokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika jimbo hilo.
Ends


إرسال تعليق