MUSWADA MPYA WA MAREKEBISHO YA SHERIA WAFIKA BUNGENI
...Mwanasheria Mkuu awasilisha mapendekezo kwa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria
Na Joseph Ngilisho | DODOMA
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amewasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria maelezo ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2026.
Muswada huo, unaojulikana kwa Kiingereza kama The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2) Bill, 2026, unalenga kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali zinazosimamia masuala muhimu ya utawala, matumizi ya ardhi, serikali za mitaa, usalama wa Taifa, uthamini na uhifadhi wa wanyamapori.
Johari aliwasilisha maelezo hayo jana, Agosti 11, 2026, mbele ya Kamati hiyo iliyokuwa ikifanya kazi zake katika Ofisi za Bunge, jijini Dodoma.
Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kupitia na kuboresha mifumo ya kisheria ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiutawala na utekelezaji wa majukumu ya taasisi mbalimbali za umma.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria kadhaa zikiwamo Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura ya 166.
Sheria nyingine zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287, pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.
Aidha, marekebisho yanahusisha Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61, Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura ya 138, na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283.
Marekebisho hayo yanagusa maeneo yenye umuhimu mkubwa katika uendeshaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan katika usimamizi wa ardhi, mamlaka za serikali za mitaa, masuala ya usalama wa Taifa, shughuli za uthamini pamoja na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori.
Baada ya kuwasilishwa kwa maelezo hayo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), ilipokea na kujadili maelezo ya Serikali kuhusu muswada huo.
Majadiliano ya kamati hiyo ni sehemu ya mchakato wa Bunge wa kuupitia muswada huo kabla ya hatua zinazofuata za kisheria, kwa kuzingatia umuhimu wa marekebisho yanayopendekezwa katika sheria hizo.
Muswada huo unatarajiwakuwa sehemu ya hatua za Serikali katika kuimarisha mazingira ya kisheria na kuhakikisha sheria zinaendelea kuwa na ufanisi katika kukidhi mahitaji ya kiutawala, kiuchumi na kijamii nchini.
Ends.










Post a Comment