Ad
Breaking🔥

DIWANI MSTAAFU NA WENZAKE WABISHA HODI KWA MAKONDA ,WADAI KUDHULUMIWA ARDHI YA FIDIA NA JIJI LA ARUSHA,WAMLILIA AWASAIDIE AAHIDI KULIVALIA NJUGA ILI HAKI IPATIKAME .

DIWANI MSTAAFU, WENZAKE WAMLILIA MAKONDA KUPATA HAKI YA ARDHI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

DIWANI mstaafu wa Kata ya Sokoni One, Saruni Olodi, na wenzake wamebisha hodi kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, wakimlilia awasaidie kupata haki yao ya fidia ya ardhi, wakidai Halmashauri ya Jiji la Arusha imepuuza makubaliano ya maandishi yaliyofikiwa nao baada ya kuondoa kesi iliyokuwa mahakamani.


Olodi na wenzake wanadai kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha iliwaahidi kwa maandishi kuwapatia ardhi yenye ukubwa wa ekari moja kama fidia, baada ya wao kukubali kuondoa kesi iliyokuwa mahakamani kuhusu madai ya fidia katika mgogoro wa eneo lililokuwa likihusishwa na kituo cha Huruma Vision.

Kwa mujibu wa Olodi, yeye na wenzake wanane walikuwa wakiwakilisha wananchi wenzao katika kufuatilia madai ya fidia yaliyotokana na mgogoro wa eneo hilo.

Amesema makubaliano ya kuwaondoa katika shauri hilo yalipitia katika timu ya majadiliano, Kamati ya Menejimenti ya Jiji (CMT), Kamati ya Fedha pamoja na Baraza la Madiwani, hatua iliyowapa imani kuwa ahadi waliyopewa ingetimizwa.

Hata hivyo, amesema baada ya wao kuondoa kesi mahakamani, wanadai Halmashauri haikutekeleza makubaliano hayo, jambo alilolieleza kuwa limewaweka katika hali ya kukata tamaa na kulazimika kutafuta msaada wa viongozi wa Serikali.

“Nasikitika kwamba makubaliano yetu na Halmashauri ya Jiji la Arusha yaliyobarikiwa kupitia timu ya majadiliano, CMT, Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani ili tufute kesi, yamepuuzwa baada ya kufuta kesi. Huo ni utapeli wa kuaminika,” amesema Olodi.

Olodi amesema hali hiyo inawafanya kuhoji namna maazimio yanayopitishwa na vikao halali vya Jiji yanavyotekelezwa, akidai kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakifumbia macho suala hilo.

“Baraza la Madiwani pamoja na wajumbe wa Kamati ya Fedha wakiendelea kufumbia macho ukiukwaji wa kanuni, taratibu na sheria kwa kutotekeleza maazimio ya vikao halali, ni bora madiwani wote wafukuzwe na Baraza livunjwe, kwani hawana meno na hakuna la maana walilofanya pale Jiji,” amesema.

Amesema wao hawadai upendeleo bali wanataka utekelezaji wa makubaliano ambayo, kwa mujibu wake, yalifikiwa kupitia vikao na taratibu rasmi za Halmashauri.

“Hatukuondoa kesi kwa sababu hatukuwa na madai. Tulikubali kuiondoa baada ya kupewa ahadi ya maandishi kuhusu fidia ya ardhi. Tunachohitaji sasa ni utekelezaji wa kile tulichoahidiwa,” amesema.

MAKONDA AWAHAIDI KUSHUGHULIKIA

Baada ya mazungumzo mafupi na walalamikaji hao yaliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Engarenarok, jijini Arusha, ambako Makonda alikuwa amealikwa, Mbunge huyo aliwaahidi kulifanyia kazi suala lao kwa kina.

Makonda, ambaye aliwasikiliza walalamikaji hao baada ya kueleza kilio chao kuhusu madai ya fidia ya ardhi, aliwaahidi kulifuatilia jambo hilo ili kubaini ukweli wa makubaliano yaliyofikiwa na Halmashauri na kuhakikisha wanapata haki yao kwa mujibu wa taratibu.

Walalamikaji hao wamesema wamefarijika na ahadi hiyo, wakieleza kuwa walifika wakiwa na masikitiko makubwa kutokana na muda mrefu walioutumia kufuatilia suala hilo.

Olodi amesema matumaini yao sasa ni kuona suala hilo likifanyiwa kazi na kupata ufumbuzi, akisisitiza kuwa wanachodai ni utekelezaji wa makubaliano ambayo wanadai yalifikiwa na Halmashauri kupitia vikao vyake halali.

Hata hivyo, madai ya Olodi na wenzake pamoja na tuhuma dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha ni madai ya walalamikaji, hivyo upande wa Halmashauri unapaswa kutoa ufafanuzi kuhusu makubaliano hayo, maazimio yanayodaiwa kupitishwa na sababu za kutotekelezwa kwake.Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa jiji la Arusha John Kayombo ili kutoa ufafanuzi zinaendelea .

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post