Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeonya matumizi yasiyodhibitiwa ya akili bandia (AI) katika mitihani na tathmini za elimu, ikisema teknolojia hiyo inaweza kuwa chachu ya kuboresha ubora wa elimu, lakini pia ikageuka kuwa chanzo kipya cha udanganyifu na kudhoofisha uaminifu wa mitihani.
Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, Agosti 17,2026 alipomwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, katika ufunguzi wa Mkutano wa 42 wa Mwaka wa Chama cha Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), unaofanyika jijini Arusha.
Profesa Nombo alisema kasi ya maendeleo ya teknolojia inawalazimu waendeshaji wa mitihani kuimarisha mifumo ya usalama sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia, ili kuzuia AI, simu janja na mitandao ya kijamii kutumiwa kuvuruga uadilifu wa tathmini.
“Elimu ni uwekezaji mkubwa zaidi katika mustakabali wa Afrika, na tathmini ni dira inayotuonyesha kama uwekezaji huo umejengwa juu ya ubora, usawa na uadilifu,” alisema.
Alisema hakuna mfumo wa elimu unaoweza kudai ubora bila kuwa na mfumo wa tathmini unaoaminika na wenye uwezo wa kupima maarifa, umahiri, ubunifu, fikra tunduizi na uwezo wa kutatua matatizo.
Kwa mujibu wa Serikali, matumizi ya simu janja, mitandao ya kijamii na AI yameongeza changamoto katika usimamizi wa mitihani, huku mbinu za udanganyifu zikizidi kuwa za kisasa.
Hata hivyo, Profesa Nombo alisema teknolojia hiyo hiyo inaweza kutumika kukabiliana na changamoto hizo endapo itasimamiwa kwa weledi na kuzingatia maadili.
“Teknolojia hizi zinapokuwa tishio, zinaweza pia kuwa sehemu ya suluhisho,”
Alisema mabaraza ya mitihani yanapaswa kuwekeza katika mifumo imara ya usalama wa kidijitali, uchanganuzi wa data na zana zinazotumia AI kubaini kasoro na vitendo visivyo vya kawaida katika mitihani.
Alisisitiza kuwa AI haipaswi kuchukuliwa kama mbadala wa uamuzi wa kitaalamu wa wataalamu wa elimu, bali itumike kama chombo cha kuongeza ufanisi, usawa na ubora wa tathmini.
Kwa mujibu wa Serikali, matumizi ya AI katika elimu yanapaswa kuongozwa na maadili, uwazi, ulinzi wa taarifa binafsi, usawa na ujumuishi ili teknolojia hiyo isije ikazalisha pengo jipya katika upatikanaji wa elimu bora.
Serikali imezitaka mamlaka za mitihani kuimarisha usalama katika mnyororo mzima wa tathmini, kuanzia uandaaji wa maswali, uchapishaji, usafirishaji na uhifadhi hadi usimamizi wa mitihani, usahihishaji, uchakataji na utoaji wa matokeo.
Profesa Nombo alisema hatua hizo ni muhimu kwa sababu uadilifu wa mitihani ndio msingi wa kuaminika kwa vyeti na sifa za kitaaluma zinazotolewa na mifumo ya elimu.
“Uadilifu wa mitihani unabaki kuwa nguzo kuu ya uaminifu wa sifa zetu na imani ambayo jamii inaweka katika mifumo yetu ya elimu,” alisema.
Alisema mabaraza ya mitihani hayapaswi kuishia katika kusimamia mitihani ya kitaifa pekee, bali yanapaswa kuzalisha ushahidi na takwimu zitakazosaidia walimu kuboresha ufundishaji, kuwawezesha wanafunzi katika safari yao ya elimu na kuisaidia Serikali kufanya maamuzi kuhusu sera, mitaala na maboresho ya elimu.
Katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), Dkt Ashetu Kebede Gichoro amezitaka nchi za Afrika kuharakisha mageuzi ya mifumo ya tathmini kwa kutumia teknolojia na AI, akionya kuwa bara hilo likichelewa linaweza kujikuta likiwa mtumiaji wa mifumo ya nje isiyoakisi mahitaji na uhalisia wake.Alisema AI inaweza kubadili kwa kiasi kikubwa namna tathmini za elimu zinavyofanyika, ikiwamo kuwezesha mitihani inayobadilika kulingana na uwezo wa mwanafunzi, uchambuzi wa takwimu na kujenga njia binafsi za ujifunzaji.
Hata hivyo, alisema matumizi hayo yanaibua changamoto za usawa, maadili na umiliki wa data, hivyo Afrika inapaswa kujenga mifumo yake huru na salama ya kiteknolojia.
“Kama Afrika haitajenga mfumo wake huru wa tathmini uliojumuisha teknolojia, tunahatarisha kuwa watumiaji wa mifumo iliyoagizwa kutoka nje ambayo haiakisi uhalisia wetu wala kutumikia matarajio yetu,”
Alisema changamoto nyingine inayolikabili bara hilo ni matumizi duni ya takwimu za tathmini ya elimu katika kutengeneza sera na kupanga maendeleo.
Kwa mujibu wake, upungufu wa miundombinu ya kidijitali, ubora hafifu wa data na kutounganishwa kwa takwimu katika mifumo ya sera na mipango ni miongoni mwa vikwazo vinavyopunguza kasi ya maendeleo ya elimu barani Afrika.
Rais huyo alisema dunia inaingia katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na Afrika haina nafasi ya kusita katika kuunganisha teknolojia na mifumo ya tathmini.
Alisema baadhi ya maeneo ya Asia yameanza kutumia mifumo ya kidijitali na tathmini zinazoendeshwa na AI, hatua inayowasaidia wanafunzi kujiandaa kwa ushindani wa kikanda na kimataifa.
“Dunia inakwenda kwa kasi isiyokuwa ya kawaida na Afrika haiwezi kumudu kusita au kutoa visingizio. Wito ni wa haraka, jukumu ni letu na wakati wa kuchukua hatua ni sasa,”.
Alisema AEAA inapaswa kuwa taasisi ya bara inayowezesha kujengwa kwa mifumo ya tathmini inayostahimili misukosuko, inayolenga mustakabali na inayounganisha teknolojia, huku ikiwa ya Kiafrika, huru na yenye kuaminika kimataifa.
Akizungumzia ushirikiano wa Afrika, Ashetu alirejea falsafa za Medemer ya Ethiopia na Ujamaa ya Tanzania, akisema misingi yake inasisitiza mshikamano, umoja, kufanya kazi pamoja na kujenga uwezo wa kujitegemea.
Amesema falsafa hizo zinaweza kuwa msingi wa kujenga mfumo wa pamoja wa tathmini za elimu barani Afrika.
Alitumia methali kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kusisitiza nguvu ya umoja, ikiwamo methali ya Ethiopia inayosema nyuzi za buibui zinapoungana zinaweza kumfunga simba.
“Ushirikiano, ujumuishaji, uboreshaji na mageuzi si mambo ya hiari. Ndiyo masharti ya mafanikio na ustawi wetu,” alisema.
Alitoa wito kwa AEAA, kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU), washirika wa maendeleo na vyuo vikuu, kujenga mfumo imara wa tathmini unaoweza kutumika katika maeneo yote ya bara.
Alisema mfumo huo unapaswa kuunganisha Afrika Mashariki, Magharibi, Kati, Kaskazini na Kusini, ili wanafunzi wa Afrika wasiandaliwe tu kukabiliana na mustakabali, bali wawe na uwezo wa kuwa sehemu ya kuutengeneza.
Katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohamed amewataka washiriki kutumia fursa ya kukutana Arusha kujenga uzoefu, kumbukumbu na mahusiano, akisema furaha ya kweli ya binadamu haijengwi zaidi na umiliki wa mali bali uzoefu na mahusiano mema.Alisema tafiti za saikolojia zinaonyesha kuwa watu wanaowekeza katika uzoefu na kujenga kumbukumbu wana uwezekano mkubwa wa kupata furaha kuliko wanaojikita zaidi katika kununua vitu vya mali.
“Mtu anayechagua kununua uzoefu au kujenga kumbukumbu anaaminika kuwa mwenye furaha zaidi kuliko anayechagua kununua vitu vya mali,” alisema.
Profesa Mohamed aliwashukuru washiriki kwa kuichagua Tanzania na kufika Arusha, akisema mikutano ya kimataifa si majukwaa ya kujadili taaluma pekee, bali pia hujenga mitandao ya kitaalamu, urafiki na ushirikiano baina ya nchi.
Akigusia afya barani Afrika, alisema changamoto za kiafya katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeendelea kuchangia viwango vya vifo kuwa juu na umri wa kuishi kuwa chini ya wastani wa dunia.
“Kila pumzi ni mwaliko wa kushukuru,” alisema.
Mkutano huo wa 42 wa AEAA unaongozwa na kaulimbiu “Rethinking Educational Assessment in Africa in the Age of AI”, inayolenga kutafakari upya mifumo ya tathmini ya elimu barani Afrika katika kipindi ambacho akili bandia inazidi kubadili sekta ya elimu duniani.
Mkutano huo umewakutanisha wataalamu na viongozi wa tathmini ya elimu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa ajili ya kujadili changamoto, fursa na mikakati ya kujenga mifumo ya tathmini itakayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia bila kupoteza misingi ya uadilifu, usawa, haki na ubora wa elimu.
Ends.



إرسال تعليق