Breaking🔥

PESHA ATAKA MAAFISA RASILIMALI WATU AFRIKA KUONGOZA MAPINDUZI YA NGUVU KAZI

MAAFISA RASILIMALI WATU AFRIKA WATAKIWA KUONGOZA MAPINDUZI YA NGUVU KAZI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MAAFISA Rasilimali Watu barani Afrika wametakiwa kuongoza mapinduzi ya nguvu kazi kwa kuwekeza katika maarifa, ujuzi, ubunifu na teknolojia ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu, mabadiliko ya kiteknolojia na ushindani unaoongezeka katika soko la ajira duniani.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 19, 2026, na Katibu Tawala Msaidizi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mosses Pesha, wakati akifungua rasmi Mkutano wa Pili wa Maafisa Rasilimali Watu Afrika, unaofanyika jijini Arusha.

Pesha amesema ushindani na ustawi wa mataifa ya Afrika katika uchumi wa dunia hautategemea rasilimali za asili pekee, bali utaamuliwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wa nchi kuandaa nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko.

Amesema hali hiyo inahitaji nchi za Afrika kuwa na dhamira ya pamoja ya kuimarisha rasilimali watu, kukuza ubunifu na kuandaa nguvu kazi inayoweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na lijalo.

“Mkutano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya Afrika ya kuibadilisha na kuimarisha nguvu kazi yake kupitia uwekezaji katika elimu, ukuzaji wa ujuzi, ubunifu na teknolojia endelevu, kama msingi wa kujenga nguvu kazi yenye tija, ushindani na iliyo tayari kukabiliana na mahitaji ya siku zijazo,” amesema Pesha.

Amesema maendeleo ya teknolojia na mabadiliko katika mazingira ya kazi yanapaswa kuwa kichocheo cha mataifa ya Afrika kubuni mifumo mipya ya kuwaandaa wafanyakazi, badala ya kusubiri mabadiliko yatokee na kisha kuanza kuyafanyia kazi.

Kwa mujibu wa Pesha, wataalamu wa rasilimali watu wana nafasi kubwa katika kuhakikisha nguvu kazi ya Afrika inakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kiuchumi na kijamii, kwa kuunganisha elimu, ujuzi, ubunifu na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Ameutaka mkutano huo kuwa jukwaa la majadiliano yenye tija na hatimaye kuzalisha maazimio yanayotekelezeka, yatakayosaidia kujenga ushirikiano imara miongoni mwa nchi za Afrika katika kuandaa nguvu kazi yenye uwezo wa kuchochea ukuaji shirikishi na maendeleo endelevu.

“Ni matarajio yangu kwamba mkutano huu utakuwa chachu ya majadiliano yenye tija na kutoa maazimio yanayotekelezeka, yatakayoendelea kujenga ushirikiano imara utakaobadilisha nguvu kazi ya Afrika na kuendeleza ukuaji shirikishi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja katika bara letu,” amesema.

Aidha, Pesha amewapongeza waandaaji wa mkutano huo kwa kuichagua Arusha kuwa mwenyeji, akisema hatua hiyo inaipa fursa Tanzania na Mkoa wa Arusha kuendelea kuwa kitovu cha mikutano ya kikanda na kimataifa.

Amewakaribisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika kutembelea na kufurahia vivutio vya Arusha, huku akisisitiza kuwa ukarimu wa wananchi na mazingira mazuri ya mji huo ni sehemu ya thamani inayotolewa na Tanzania kwa wageni wake.

Mkutano huo umeandaliwa na Tanzania Human Resource and Administration Professionals Association (THRAPA) kwa kushirikiana na African Human Resources Confederation (AHRC) na umewakutanisha wataalamu na Maafisa Rasilimali Watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Mkutano huo wa siku nne unaofanyika kuanzia Agosti 19 hadi 22, 2026, unajadili namna ya kubadilisha na kuimarisha nguvu kazi ya Afrika ili iweze kukidhi mahitaji ya dunia ya sasa na siku zijazo.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu “Transforming Africa Workforce for the Future”, inayolenga kusukuma ajenda ya kujenga nguvu kazi yenye tija, ubunifu, ushindani na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia.








Post a Comment

أحدث أقدم