PALLANGYO ATOA WITO WA HAKI, USALAMA WA WANANCHI TANZANIA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mfanyabiashara wa kimataifa mwenye asili ya Tanzania na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa makampuni yanayofanya shughuli katika sekta mbalimbali, Ombeni Pallangyo, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, vifo vya raia na vitendo vya vyombo vya dola vinavyodaiwa kuhatarisha usalama wa wananchi nchini Tanzania.Pallangyo, ambaye anaendesha shughuli za biashara katika sekta za usafirishaji wa kimataifa, utalii wa ikolojia, huduma za ukarimu pamoja na shughuli za kijamii kupitia taasisi zake za misaada, amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka kutoka kwa mamlaka za Tanzania na jumuiya ya kimataifa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Agosti 16, 2026, Pallangyo ameeleza kuwa ameamua kuzungumza hadharani kutokana na kile alichokiita kuongezeka kwa matukio ya vifo vya raia katika maeneo yanayopakana na hifadhi pamoja na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na vitendo vya polisi dhidi ya wananchi.
Amesema anazungumza kama Mtanzania anayewekeza nchini, anayeajiri vijana na wanawake na anayeshiriki kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia shughuli zake za biashara na kijamii.
“Nazungumza leo si tu kama kiongozi wa kampuni ya kimataifa, bali kama mwana wa Tanzania ninayeamini kwa kina katika watu wetu na uwezo mkubwa wa taifa letu. Uzalendo wa kweli unatutaka kusimama pale utu na maisha ya binadamu vinapokuwa hatarini,” amesema Pallangyo.
Amesema ukimya haupaswi kuwa chaguo wakati maisha ya watu wasio na hatia yanapotea na wananchi wanaishi kwa hofu ya wale wanaopaswa kuwa walinzi wao.
Pallangyo pia amedai kuwa amewahi kukumbana na tukio alilolielezea kuwa ni kutekwa kinyume cha sheria na polisi jijini Arusha, akisema tukio hilo limeongeza msukumo wake wa kutaka uwajibikaji wa vyombo vya dola na ulinzi wa haki za raia.
Katika taarifa hiyo, mfanyabiashara huyo amesema anachukua hatua za kuwasilisha taarifa na malalamiko yake kwa taasisi za kidiplomasia za kimataifa pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akitaka madai hayo yachunguzwe kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanapata uchunguzi huru na wa kuaminika, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya raia na kuheshimu utawala wa sheria.
Pallangyo amewataka viongozi wa Tanzania kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka na kwamba matukio yanayodaiwa kusababisha vifo au mateso kwa raia yanachunguzwa bila upendeleo.
Hata hivyo, katika taarifa hiyo hakutoa maelezo ya kina kuhusu jalada au nyaraka alizowasilisha katika taasisi hizo za kimataifa, wala hakutajwa majibu ya mamlaka za Tanzania kuhusu madai hayo.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu usalama wa wananchi, matumizi ya nguvu na uwajibikaji wa vyombo vya dola ukiendelea kuwa suala linalohitaji uchunguzi na majibu kutoka kwa mamlaka husika.
Post a Comment