MLIMA WA TAKA WAPOROMOKA, WATU 30 WAFARIKI GUINEA
By Arushadigital
CONAKRY, Guinea — Takribani watu 30 wamefariki dunia na wengine 22 kujeruhiwa baada ya mlima wa taka kuporomoka na kuangukia nyumba zilizokuwa jirani, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika mji mkuu wa Guinea, Conakry.
Tukio hilo limetokea majira ya saa nane usiku katika eneo la Dar es Salaam jijini Conakry, huku mamlaka zikisema dampo hilo liliporomoka ghafla baada ya mvua kubwa, na kusababisha vifusi kuangukia nyumba na watu waliokuwa wamelala.
Serikali ya Guinea imetuma vikosi vya usalama, likiwemo jeshi, kushiriki katika shughuli za uokoaji na kuwatafuta watu wanaodhaniwa kuwa wamefunikwa na vifusi.
Shuhuda mmoja wa kike ameliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa watoto wake watano wamefariki dunia katika ajali hiyo, hali inayoonyesha ukubwa wa janga hilo.
Mamlaka zinaendelea na operesheni ya uokoaji, huku kukiwa na hofu kwamba watu wengine bado wamekwama chini ya vifusi na hivyo idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Waziri Mkuu wa Guinea, Amadou Ouari Ba, ametembelea eneo la tukio na kukagua shughuli za uokoaji pamoja na hali ya waathiriwa.
Awali, kiongozi wa eneo hilo, Lansine Sila, aliliambia Shirika la Habari la AFP kuwa kulikuwa na hofu ya idadi kubwa ya waathiriwa. Alisema hadi wakati huo miili 18 ilikuwa imepatikana na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Ends

إرسال تعليق