Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
AFISA Elimu wa Halmashauri ya Meru, Mariam Mgonja, amewataka wazazi kuacha dhana kwamba malezi ya mtoto ni jukumu la shule pekee, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu na jamii ni nguzo muhimu katika kumjenga mtoto mwenye elimu, nidhamu na maadili.Mgonja alisema hayo leo Agosti 22,2026 wakati alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya Darasa la Saba ya Rays Pre and Primary School, iliyopo Kijiji cha Nasholi, Kata ya Kikatiti, Halmashauri ya Meru, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Alisema pamoja na wazazi kuwekeza fedha na nguvu katika elimu ya watoto wao, wanapaswa kuwekeza kwa kiwango hicho hicho katika malezi na maadili, kwa kuwa elimu isiyoambatana na nidhamu inaweza kushindwa kutoa matokeo yanayotarajiwa katika maisha ya mtoto.“Wazazi mmewekeza sana katika elimu ya watoto wenu. Kila mzazi anatamani mtoto wake asome kwa sababu elimu ni uwekezaji. Lakini pamoja na uwekezaji huo, naomba tuwekeze pia kwenye maadili,” alisema.
Mgonja alisema mtoto anapokuwa shuleni huwa chini ya uangalizi wa walimu kwa muda maalumu, lakini sehemu kubwa ya maisha yake hutumia nje ya shule, hivyo wazazi wana wajibu mkubwa wa kufuatilia mwenendo wake.
Aliwataka wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao, kufahamu wanakokwenda, marafiki wanaoshirikiana nao na shughuli wanazofanya baada ya kutoka shuleni, akisema uangalizi huo ni sehemu ya msingi ya kumlinda mtoto dhidi ya mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wake.“Katika safari ya mtoto kutoka shuleni mpaka jioni kuna mambo mengi ambayo mtoto wetu anakutana nayo. Nawaomba tuwe karibu na watoto wetu pamoja na majukumu na harakati tunazopambana nazo kutafuta fedha huku na kule,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mgonja aliwataka wazazi kuongeza umakini katika usalama wa watoto wao, akisema si kila mtu anayekuja nyumbani au anayejitambulisha kama ndugu anapaswa kuaminiwa bila tahadhari.
Alisema wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanaachwa katika mazingira salama na chini ya uangalizi wa watu wanaoaminika, kwa kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaweza kufanywa hata na watu walio karibu na familia.
“Tusiamini kila mtu anayekuja nyumbani kwetu kwa sababu tu ni mjomba, baba mdogo au ndugu. Tuwe makini sana. Huwezi kujua moyo wa mtu umebeba nini,” alisema.
Mgonja pia aliwataka wazazi kuendelea kuunga mkono programu za afya kwa watoto, ikiwemo chanjo zinazotolewa na Serikali, huku akiwashauri kutegemea taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya badala ya taarifa zisizo na msingi zinazoweza kuhatarisha afya za watoto.
Alisema kuhitimu Darasa la Saba si mwisho wa safari ya elimu wala maisha, bali ni mwanzo wa hatua nyingine inayowahitaji watoto hao kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika mazingira mapya watakayokutana nayo.
“Malezi mazuri mliyoyapata hapa Rays yasiishie hapa. Yafanyeni kuwa nguzo yenu huko mtakakokwenda. Mkienda shule nyingine, mkutane na mazingira mapya au watu wapya, msiyasahau maadili mliyofundishwa hapa,” alisema.
Alisema matarajio ya Serikali ni kuona shule hiyo ikiendelea kukua kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaohitimu na kufanya mitihani ya kitaifa, huku ikiendelea kudumisha viwango vya elimu na malezi.
Mgonja aliipongeza shule hiyo kwa kufikia hatua ya kufanya mahafali yake ya kwanza ya Darasa la Saba, akisema mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, wazazi, walimu na jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rays Pre and Primary School, Naiman Shami, aliiomba Serikali kuendelea kushirikiana na shule binafsi katika kuhakikisha watoto wanapata elimu na malezi bora, huku akitaka shule hizo zipewe usimamizi wa haki na usawa katika mitihani.
Shami alisema shule binafsi zinafanya sehemu kubwa ya kazi ya kutoa elimu kwa Watanzania na zinahitaji ushirikiano wa karibu na Serikali ili uwekezaji unaofanywa na wazazi na shule uwe na matokeo yanayotarajiwa.
“Tunajua tuna munganiko na tunashirikiana na Serikali kwa ajili ya watu. Tuna mitihani mbalimbali, tunaomba sisi shule binafsi pia msitusahau kwa chochote. Tunapokuwa na mitihani tupewe usimamizi wa haki na usawa,” alisema.
Alisema mazingira ya mitihani yanapaswa kuwa ya haki ili kila mwanafunzi apate nafasi ya kuonyesha uwezo wake halisi bila kujali kama anatoka shule binafsi au ya Serikali.
“Leo tunaona watoto wetu wanagraduate na tumeona jinsi ambavyo shule yetu imekuwa ikiendelea na kutunza watoto wetu,” alisema.
Alisema shule itaendelea kuwekeza katika elimu, malezi na makuzi ya watoto, huku akiwataka wazazi kuendelea kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha nafasi za walimu wanaoondoka zinajazwa kwa wakati.
“Tunahitaji wale wadogo zetu, walimu wengine wakaweza kufikia haya mapengo ya hawa wanaoondoka. Waleteni, tuchague ili tuweze kwenda sambamba,” alisema
Alisema Rays ilisajiliwa mwaka 2024 na kuanza rasmi kutoa huduma za elimu Januari 2025, ikiwa sasa na takribani wanafunzi 400, kuanzia ngazi ya chekechea hadi shule ya msingi.
Elirehema alisema shule hiyo imejikita katika kuwajenga wanafunzi kitaaluma, kimaadili, kijamii na kihisia ili kuwaandaa kwa hatua nyingine ya elimu na maisha.
“Kwa wahitimu wetu, hongereni sana. Hii siyo mwisho wa safari yenu, bali ni mwanzo wa safari kubwa zaidi. Endeleeni kuwa na nidhamu, heshima, bidii na kiu ya kujifunza,” alisema.
Alisema shule itaendelea kuboresha viwango vya ufundishaji na malezi, huku akiwashukuru wazazi kwa kuiamini Rays na walimu kwa kujituma katika kuwafundisha na kuwalea watoto.
Mahafali hayo yamekuwa ya kihistoria kwa Rays Pre and Primary School kwa kuwa ni mahafali ya kwanza ya Darasa la Saba tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, yakihitimisha safari ya kundi la kwanza la wanafunzi wa shule hiyo katika elimu ya msingi.
Rays Pre and Primary School ipo Kijiji cha Nasholi, Kata ya Kikatiti, Halmashauri ya Meru, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, takribani kilomita mbili kutoka Barabara Kuu ya Arusha–Moshi, na inatoa elimu ya awali na msingi kwa mchepuo wa Kiingereza.
NDOSI: RAYS INAJENGA KIZAZI CHA KUJIAMINI




















Post a Comment