TAKUKURU YAMKAMATA RAIA WA ROMANIA KWA TUHUMA ZA KUTENGENEZA KADI BANDIA ZA BENKI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha inamshikilia raia wa Romania, Constantin Catalin Podoleanu (39), kwa tuhuma za kutengeneza na kutumia kadi bandia za benki katika kufanya miamala ya fedha kutoka kwenye akaunti za watu wengine.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 20, 2026, majira ya saa 4:00 usiku, katika eneo la Njiro, Jijini Arusha, katika operesheni iliyofanywa na maafisa wa TAKUKURU.
Baada ya kukamatwa, maafisa hao walifanya upekuzi katika makazi yake yaliyopo Njiro Block D, Kata ya Engutoto, ambapo walidaiwa kukuta vifaa mbalimbali vinavyodhaniwa kutumika katika kutengeneza na kuendesha shughuli za kadi bandia za benki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema upekuzi huo ulifanikisha kukamatwa kwa vifaa mbalimbali, vikiwemo mashine sita za POS, kadi mbalimbali za benki, kompyuta mpakato mbili, pamoja na vifaa na kemikali zinazodaiwa kutumika katika utengenezaji wa kadi hizo.
FEDHA, STAKABADHI ZENYE THAMANI KUBWA ZAKAMATWA
Mbali na vifaa hivyo, TAKUKURU imebaini pia Sh milioni 2.17 taslimu, fedha za kigeni pamoja na stakabadhi za malipo zenye thamani ya takribani Sh milioni 171.7 na Dola za Marekani 55,987.20.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, baadhi ya taarifa zilizobainika kwenye kadi zinazodaiwa kutumika katika miamala hiyo zinahusishwa na raia wa mataifa mbalimbali nje ya Tanzania.
TAKUKURU inadaiwa kubaini kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti za watu hao zilitumika kufanya malipo ya huduma mbalimbali nchini Tanzania, huku wamiliki wa akaunti hizo wakidaiwa kutokuwa na taarifa wala kuhusika na huduma zilizolipiwa katika kipindi ambacho miamala hiyo ilifanyika.
MTANDAO WACHUNGUZWA
Taasisi hiyo imeeleza kuwa uchunguzi bado unaendelea kwa lengo la kubaini ukubwa wa mtandao huo, watu wengine wanaoweza kuhusika na namna fedha hizo zilivyokuwa zikihamishwa na kutumika.
Zawadi amesema TAKUKURU inaendelea kukusanya ushahidi na kuchunguza mazingira yote yanayohusiana na tuhuma hizo, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika kwa mujibu wa sheria.
Tukio hilo linaongeza tahadhari kuhusu matumizi ya teknolojia katika uhalifu wa kifedha, hususan katika wizi wa taarifa za kibenki, utengenezaji wa kadi bandia na matumizi yasiyoidhinishwa ya akaunti za watu wengine.
TAKUKURU imewataka wananchi kuwa makini katika kulinda taarifa zao za kibenki, kadi za benki na namba za siri, pamoja na kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika pindi wanapobaini miamala isiyo ya kawaida katika akaunti zao.
Uchunguzi wa TAKUKURU unaendelea.
Ends






Post a Comment