Breaking🔥

MAKALLA AIPA NGUVU HORTILOGISTICA AFRICA KUELEKEA JUKWAA LA UWEKEZAJI NA BIASHARA NOV 8- 2026 ARUSHA,MKINDI AHIDI JUKWAA LA KITAIFA LA KILA MWAKA

MAKALLA AIPA NGUVU HORTILOGISTICA AFRICA 2026

...Aahidi ushirikiano, ataka jukwaa lifungamanishwe na utalii, uwekezaji na uchumi wa Arusha

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, ameahidi ushirikiano wa Serikali ya Mkoa katika kufanikisha Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji na Biashara katika Sekta ya Mbogamboga, Matunda na Maua, HortiLogistica Africa 2026, akilitaka liunganishwe na fursa za utalii, uwekezaji na uchumi wa mkoa huo.

Makalla ametoa ahadi hiyo leo, Agosti 10, 2026, alipokutana na Mtendaji Mkuu wa  Sekta binafsi  ya Horticulture nchini (TAHA), Dk. Jacqueline Nkindi,pamoja na ujumbe wake, waliowasilisha rasmi mpango wa maandalizi ya jukwaa hilo.

Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2026, katika Ukumbi wa Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha, likilenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya mbogamboga, matunda na maua kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza baada ya kupokea wasilisho hilo, Makalla alisema Serikali ya Mkoa ipo tayari kushirikiana na TAHA kuhakikisha jukwaa hilo linafanyika kwa mafanikio na linazalisha matokeo yatakayowanufaisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na uchumi wa Arusha kwa ujumla.

Alisema tukio hilo si la sekta ya kilimo pekee, bali lina nafasi ya kuibua mnyororo mpana wa shughuli za kiuchumi, ikiwamo usafirishaji, huduma za kifedha, teknolojia, utalii, malazi na masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Jambo hili linaipa heshima nchi yetu na Rais wetu kwa kuwaleta wadau wote wa mbogamboga, matunda na maua Arusha. Lakini pia ukitafuta tija ya jambo hili kiuchumi, mnyororo wake ni mkubwa. Kwa hiyo mimi kama Mkuu wa Mkoa, itoshe kusema kwamba sasa tunaanza safari pamoja ya kufanikisha jambo hili,” alisema Makalla.

Makalla alisema kutokana na nafasi ya Arusha katika sekta ya utalii na mikutano ya kimataifa, jukwaa hilo linapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na kuunganisha wazalishaji na masoko makubwa ya kimataifa.

Alisema ushirikiano huo unapaswa kwenda zaidi ya kufanikisha tukio la Novemba, bali kujenga mfumo endelevu ambao utalifanya jukwaa hilo kuwa sehemu muhimu ya kukuza uwekezaji, biashara na ajira katika sekta ya kilimo na sekta nyingine zinazohusiana nayo.

TAHA YAJA NA SOKO LA KIMATAIFA

Kwa upande wake, Dkt. Mkindi alisema HortiLogistica Africa 2026 inalenga kuwa jukwaa la kimataifa litakalofanyika kila mwaka mkoani Arusha, likiwaunganisha wadau muhimu katika mnyororo wa thamani wa mbogamboga, matunda na maua.

Alisema jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha wanunuzi wakubwa wa mazao, wazalishaji, wawekezaji, kampuni za teknolojia, wasafirishaji, taasisi za fedha na wadau wengine wa biashara kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Dkt. Mkindi, uwepo wa wadau hao unatarajiwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa Tanzania kupata masoko mapya, kujenga mahusiano ya kibiashara na kuvutia mitaji pamoja na teknolojia zitakazosaidia kuongeza tija katika uzalishaji.

Aidha, jukwaa hilo linatarajiwa kutoa nafasi ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwamo upatikanaji wa masoko, teknolojia, fedha, miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mazao, pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kufikia masoko ya kimataifa.

ARUSHA KITUO CHA BIASHARA

Uamuzi wa kulifanya Arusha kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo unaongeza nafasi ya mkoa huo kuendelea kujijenga kama kituo cha mikutano, biashara na uwekezaji wa kimataifa.

Kwa kulifungamanisha HortiLogistica Africa 2026 na utalii, Serikali ya Mkoa inatarajiwa kutumia uwepo wa wageni wa kimataifa kuongeza matumizi katika hoteli, usafiri, migahawa, huduma za kitaalamu na biashara nyingine zinazotegemea sekta ya mikutano na utalii.

Hivyo, jukwaa hilo linaweza kuwa zaidi ya mkutano wa wafanyabiashara wa mbogamboga, matunda na maua, bali kuwa sehemu ya mnyororo mpana wa uchumi unaounganisha kilimo, biashara, uwekezaji, usafirishaji, teknolojia na utalii.

Kwa Arusha, tukio hilo pia linaweka mkoa katika nafasi ya kuendelea kuvutia majukwaa ya kimataifa yanayoweza kufungua milango ya mitaji, masoko na teknolojia kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم