LUKUMAY ATEMBELEA MTOTO MWENYE TATIZO LA MOYO, AANZA KUTAFUTA SULUHISHO LA UPASUAJI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
ARUSHA. Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, leo Agosti 16, 2026, ametembelea familia ya Bi. Oliver Thobias, mzazi wa mtoto Charity Tumaini Mwenyewe, anayesumbuliwa na tatizo la moyo linalohitaji kufanyiwa upasuaji.
Mtoto huyo amekuwa akikabiliwa na hali ya kuchoka mara kwa mara pamoja na kupata shida ya kupumua anapotembea au kukimbia, hali iliyolazimu familia kumpeleka katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya jijini Arusha bila kupata suluhisho.
Baada ya juhudi hizo kushindikana, madaktari walimpa rufaa kwenda Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, baada ya kufanyiwa uchunguzi katika hospitali hiyo, madaktari walibaini kuwa Charity ana tatizo la moyo linalohitaji kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo, familia imekumbwa na changamoto ya gharama za matibabu, ambapo inadaiwa kuwa zaidi ya Sh milioni tisa zinahitajika kwa ajili ya upasuaji huo.
Kutokana na kushindwa kumudu gharama hizo, familia ililazimika kumrudisha mtoto nyumbani huku ikiendelea kutafuta msaada kutoka kwa wadau na wananchi wenye uwezo wa kuchangia matibabu yake.
Dkt. Lukumay alifika nyumbani kwa familia hiyo baada ya kuona kupitia mitandao ya kijamii wito wa wananchi unaoendelea wa kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.
Lengo la ziara hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, lilikuwa kupata taarifa za kina kuhusu hali ya mtoto na changamoto zinazokabili familia, ili kutafuta njia bora ya kuwezesha mtoto huyo kupata matibabu anayohitaji.
Mbunge huyo ameeleza dhamira ya kushirikiana na familia na wadau mbalimbali katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa upasuaji ndiyo njia iliyopendekezwa na madaktari.
Hatua hiyo imekuja wakati familia ikiendelea kuomba msaada wa wananchi, taasisi na wadau mbalimbali ili kufanikisha upasuaji wa Charity na kumpa nafasi ya kurejea katika maisha ya kawaida bila kukumbwa na changamoto za kiafya anazopitia sasa.
Familia imetaja kuwa msaada wa wananchi unaendelea kuwa muhimu katika kufanikisha gharama za matibabu, huku matumaini yakielekezwa kwa wadau watakaoguswa na hali ya mtoto huyo.
Ends


Post a Comment