YANGA YATOZWA FAINI YA SH. MILIONI 100, HERSI NA MTINE WAPELEKWA KAMATI YA MAADILI
By Arushadigital
Klabu ya Young Africans (Yanga) imetozwa faini ya Sh milioni 100 baada ya kukiuka taratibu za matumizi ya chumba rasmi cha kuvalia wachezaji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Julai 2, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyotolewa Julai 3, 2026, wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Yanga walitumia nyumba iliyo nje ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, maarufu kama Jumba Jeupe, badala ya kutumia chumba rasmi cha kuvalia kilichoandaliwa ndani ya uwanja.
TPLB imeeleza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 17:20 ya Kanuni za Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo, hivyo klabu hiyo imeadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 kwa kutozwa faini ya Sh milioni 100.
Mbali na adhabu hiyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imempeleka Rais wa Yanga, Hersi Said, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa hatua zaidi zinazohusiana na tukio hilo.
TPLB pia imekumbusha kuwa si mara ya kwanza kwa Yanga kuadhibiwa kwa kosa hilo, kwani Mei mwaka huu ilitozwa faini ya Sh milioni 30 baada ya kukiuka taratibu hizo hizo.
Ends

إرسال تعليق