LISSU AOMBA RUFAA YATUPILIWE MBALI, ATAKA DPP AMLIPE FIDIA KWA UCHELEWESHAJI WA SHAHURI
By Arushadigital-Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akieleza kuwa yana lengo la kuchelewesha kesi yake ya msingi, huku akiitaka mahakama hiyo iamuru fidia kutokana na kile alichokiita usumbufu wa muda mrefu alioupata akiwa mahabusu.
Lissu ametoa kauli hiyo mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Shimiwa Mwarija, Muruke na Khamis, ambapo alidai kuwa mwenendo wa shauri hilo umecheleweshwa kwa siku 139 kwa makusudi, hali iliyochangia kuendelea kwake kuwa gerezani kwa muda wa mwaka mmoja na miezi kadhaa.
“Kwa jinsi ambavyo nimezungumza, haya maombi yameletwa kwa lengo moja tu—kurefusha kesi ya msingi. Na ukirefusha kesi ya msingi, mjibu maombi ataendelea kukaa Ukonga Prison. Leo ni siku ya 139 tangu mbinu hii ya ucheleweshaji ianze. Niko gerezani kwa mwaka mmoja na miezi mitatu, lakini ucheleweshaji huu wa siku 139 (kuanzia Februari 24, 2026 hadi Julai 3, 2026),” alieleza Lissu mahakamani.
Akiendelea kuwasilisha hoja zake, Lissu alihoji uhalali na maslahi ya umma katika maombi hayo ya DPP, akisisitiza kuwa yanaenda kinyume na misingi ya kikatiba inayotaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kusimamia haki kwa kuzingatia maslahi ya umma.
“Maombi haya yana maslahi gani ya umma?” alihoji Lissu.
Katika hoja zake za mwisho, Lissu aliiomba Mahakama ya Rufani sio tu kuyatupilia mbali maombi hayo, bali pia kutumia mamlaka yake kumuamuru DPP kumlipa fidia kwa madhara na usumbufu alioupata kutokana na kile alichodai kuwa ni ucheleweshaji wa makusudi wa shauri hilo.
“Ombi langu si tu kuyakataa maombi haya, bali pia kutumia mamlaka ya mahakama kumlazimisha mleta maombi anilipe fidia kwa taabu niliyopata kutokana na ucheleweshaji huu wa siku 139,” alisema Lissu.
Ends

إرسال تعليق