WAISLAMU TWARIQA KUANGUSHA DUA NZITO ARUSHA RAIS SAMIA AALIKWA KUONGOZA DUA, MAADHIMISHO KIFO CHA DARUWESHI MTI MKAVU KUTIKISA

 SAMIA AOMBWA KUONGOZA DUA MAALUM YA AMANI AGOSTI 21

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KATIBU Mkuu wa Taasisi ya Twariqatul Qadiriyya Arraziqiyya Al-Jaylaniyya Tanzania, Sheikh Haruna Husein, amesema taasisi hiyo imemwandikia rasmi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikimuomba kushiriki na kuongoza dua maalum ya kuliombea Taifa itakayofanyika Agosti 21 mwaka huu katika Zawiya Kuu jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya aliyekuwa kiongozi wa taasisi hiyo, Hayati Daruweshi Mtimkavu.

Akizungumza na waandishi wa habari ,jumapili Julai 12,2026 Zawiya Kuu ya taasisi hiyo jijini Arusha, Sheikh Haruna alisema maandalizi ya dua hiyo yamekamilika ambapo shughuli zitaanza mchana kwa programu maalum ya kina mama na kuendelea usiku kucha hadi alfajiri kwa ibada, dua na maombi mbalimbali.

Alisema tangu mwaka 1972, viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakishiriki katika maadhimisho hayo, akiwemo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Sheikh Haruna alisema uwepo wa Rais Samia katika dua hiyo utakuwa ishara ya kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuliongoza Taifa kwa hekima, busara na amani.

“Dua hii inalenga kumuombea Hayati Daruweshi Mtimkavu, ambaye aliacha urithi wa upendo, umoja na maridhiano, lakini pia kuliombea Taifa letu la Tanzania liendelee kuwa na amani, utulivu na mshikamano,” alisema.

Alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa, akisema viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuhubiri na kuilinda kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Aidha, Sheikh Haruna aliwataka viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na wananchi wote kushiriki katika dua hiyo, akieleza kuwa maombi ya pamoja yana nafasi kubwa katika kuimarisha umoja wa Watanzania.

Katika hatua nyingine, aliwataka wanachama wa Twariqa kuendelea kudumisha umoja na kuepuka migawanyiko inayoweza kuchochewa na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

Alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kukutana na kujenga maridhiano kwa maslahi mapana ya Taifa badala ya kuweka mbele maslahi binafsi.

“Maridhiano hayajengwi na mtu mmoja wala kwa maslahi ya kundi fulani. Yanajengwa kwa ajili ya Watanzania wote na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na yenye umoja,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Taifa kupitia Taasisi ya Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya, Khalifa Juma Salim, amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani, upendo na mshikamano akisema utulivu ndiyo msingi wa maendeleo.

Khalifa alisema amani ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowezesha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo dini, elimu, biashara na maisha ya kila siku.

Alisema jamii inapaswa kuepuka vitendo vya vurugu na migawanyiko huku akisisitiza umuhimu wa kushikamana na mafundisho ya Qurani na Sunnah pamoja na kuenzi maadili na adabu njema.

Naye Kiongozi wa Taasisi ya Kiislamu ya Twariqatul wilaya ya Arumeru, Sheikh Iddy Ngella, alisema Watanzania wanapaswa kushikamana, kusikilizana na kuheshimiana ili kulinda amani na utulivu wa Taifa.

Sheikh Ngella alisema tofauti za kisiasa ni sehemu ya ujenzi wa Taifa na vyama vinapaswa kushindana kwa hoja zenye lengo la kuleta maendeleo badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

“Tunapaswa kushikamana, kusikilizana na kuheshimiana ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani,” alisema.

Aidha, alisema baadhi ya watu wenye nia ovu wanaweza kutumia mazingira mbalimbali kuleta migawanyiko na kuharibu amani ya nchi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na kulinda umoja wa kitaifa.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuunganisha jamii kwa kutoa taarifa zinazojenga amani, utulivu na usalama wa Taifa.

Post a Comment

أحدث أقدم