KIONGOZI TWARIQARUL QADIRIYA AR-RAZIQIYA AHIMIZA AMANI, ATANGAZA MAADHIMISHO YA DARUWESHI MTIMKAVU
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Twariqarul Qadiriya Ar-Raziqiya Al-Jaylaniya Tanzania, Sheikh Haruna Husein, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano huku akitangaza ratiba ya maadhimisho ya kumbukumbu ya muasisi wa taasisi hiyo, Daruweshi Mtimkavu.
Akizungumza Julai 12, 2026, katika Makao Makuu ya taasisi hiyo, Sheikh Haruna alisema maadhimisho hayo yataanza rasmi Agosti 21, 2026 katika Zawiya Kuu, makao makuu ya taasisi hiyo, kabla ya kuendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
Alisema Daruweshi Mtimkavu alitumia maisha yake yote, yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 100, kuwalingania watu kumjua Mwenyezi Mungu, kumfuata Mtume Muhammad (S.A.W.), kuishi kwa uchamungu, uadilifu na kuacha maovu, jambo lililowafanya kuwa miongoni mwa viongozi wa dini walioacha alama kubwa katika kuimarisha imani na maadili ya jamii.
Sheikh Haruna alisema mbali na shughuli za ibada, maadhimisho ya mwaka huu yatahusisha utoaji wa damu, kutembelea wagonjwa hospitalini, kupanda miti, kuwatembelea watoto yatima pamoja na watu waliopo magerezani ili kuwajulia hali na kuwafariji, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza falsafa ya Daruweshi Mtimkavu ya kuitumikia jamii.
Aliwataka wafuasi wa Twariqa ya Qadiriya kutoka mikoa yote ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo, akieleza kuwa Zawiya Kuu ndiyo kitovu cha shughuli zote za taasisi hiyo na mahali ambapo Daruweshi Mtimkavu alianzisha na kuendesha shughuli zake za kiroho.
Katika hotuba yake, Sheikh Haruna aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, umoja na maridhiano, akisisitiza kuwa bila amani haiwezekani wananchi kutekeleza ibada, kufanya kazi na kufurahia haki zao.
"Viongozi wa dini tuna wajibu mkubwa wa kuhubiri amani. Amani ndiyo msingi wa umoja, mshikamano na maridhiano. Tukipoteza amani, hata haki itakuwa vigumu kupatikana," alisema.
Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kuilinda nchi kwa kudumisha amani na mshikamano, akisema uzoefu wa mataifa mengine yaliyokumbwa na migogoro unaonyesha kuwa amani ni hazina ambayo inapaswa kulindwa na kila mwananchi.
Ends..






إرسال تعليق