TRA YAAHIDI KUIMARISHA UKUSANYAJI WA KODI KWA HAKI, HESHIMA NA UWELEDI
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa kuzingatia misingi ya haki, heshima kwa walipakodi na weledi wa kitaaluma, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari nchini.
Akizungumza Jumatatu Julai 06,2026 wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Tathmini ya Ukusanyaji wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 jijini hapa, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, alisema maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yalikuwa ya kihistoria huku yakihudhuriwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi katika kilele cha Tuzo za Rais za Mlipa Kodi.
Alisema moja ya ajenda kuu za mkutano huo ni kuweka mikakati ya kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Rais ili kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari na kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.
Mwenda aliwashukuru walipakodi wote nchini, wadogo, wa kati na wakubwa, kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kushirikiana na TRA katika kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Alisema TRA itaendelea kuhakikisha kodi zinakusanywa kwa haki kwa kuzingatia sheria, huku kila mlipakodi akiheshimiwa na kupewa huduma bora zinazorahisisha utekelezaji wa majukumu yake ya kikodi.
Aidha, alisema mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha weledi katika usimamizi wa kodi ili kuongeza ufanisi wa huduma na kujenga mazingira yanayochochea ukuaji wa biashara.
Mwenda alisema maelekezo ya Rais yalisisitiza nguzo tatu muhimu za kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari, ambazo ni ukusanyaji wa kodi kwa haki, utoaji wa huduma kwa heshima kwa walipakodi na usimamizi wa kodi unaozingatia uelewa na weledi wa kitaaluma.
Alisisitiza kuwa TRA haitamdhulumu mlipakodi, lakini pia haitaruhusu mlipakodi kuidhulumu nchi kwa kukwepa kodi, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mmoja analipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
Alisema msingi wa kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari ni kujenga imani kati ya walipakodi na TRA kupitia usimamizi wa haki, matumizi sahihi ya mapato ya kodi na utoaji wa huduma bora zinazowezesha biashara kustawi.
Mwenda alibainisha kuwa mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yanaonyesha ushirikiano huo umezaa matunda, akieleza kuwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani makusanyo ya kodi yalikuwa takribani Sh trilioni 21 kwa mwaka, huku mwaka wa fedha 2025/2026 yakifikia Sh trilioni 37.9, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 37.
Aliwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, mawaziri mbalimbali, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa Serikali kwa ushirikiano wao katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Pia aliwapongeza watumishi wote wa TRA kwa uzalendo, uadilifu, kujituma na utoaji wa huduma bora, akisema wao ndio chachu ya mafanikio ambayo mamlaka hiyo imeyapata katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Alihitimisha kwa kuwatakia TRA mafanikio katika safari ya miaka 30 ijayo na kutangaza rasmi kufunguliwa kwa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Tathmini ya Ukusanyaji wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 akisisitiza walipakodi wasiidhulumu TRA.
Awali Mkurugenzi rasilimali watu Moshi Kabengwe alisema mkutano huo wa siku 5 utajumuisha washiriki wapatao 477 wa mamlaka hiyo pamoja na wadau wengine wa Kodi.
Alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kuendelea kuweka rekodi ya kuwa na cleansheet katika miezi 12 mfunulizo na kufanya kuwa na wastani wa asilimia 105.24 kwa mwaka wa fedha 2025/26 moja kati ya mafanikio makubwa yaliyotokea katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ,huku wakitarajia sasa kukusanya takribani trilioni 41 katika mwaka wa fedha ujao .
Ends..
.



















إرسال تعليق