PIGO CHADEMA MWENYEKITI ATIMKIA CCM, ASEMA HANA TENA HOJA YA KUIKOSOA SERIKALI

JUMBE AACHANA NA CHADEMA, ASEMA HANA TENA HOJA YA KUIKOSOA SERIKALI

Na Hadija Bagasha | TANGA

 ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe Hamza, amekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hali iliyomfanya kuona hana tena sababu ya kuendelea kuwa upande wa upinzani.


Jumbe, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CUF kabla ya kuhamia ACT-Wazalendo na baadaye CHADEMA, amekuwa mmoja wa viongozi wa upinzani waliotambulika kwa msimamo mkali dhidi ya CCM kwa takribani miaka 30 ya shughuli za kisiasa.

Alipokelewa rasmi Julai 6, 2026, katika Ofisi za CCM Mkoa wa Tanga na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abrahman Abdallah, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na wanachama wa chama hicho.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Tanga mara baada ya kupokelewa, Jumbe alisema katika kipindi chake chote cha siasa za upinzani amekuwa akiidai Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini sasa ameridhishwa kuwa malengo hayo yamefikiwa.

"Nimekuwa nikifanya siasa kwa muda wa miaka mingi, takribani miaka 30. Kila kitu nilichokuwa nakipigia kelele pamoja na wenzangu kimefanyika. Bandari ya Tanga imejengwa, barabara nyingi zimejengwa, hivyo leo najiunga na CCM kwa sababu sioni sababu ya kuendelea kuwa upande wa upinzani," alisema.

Alisisitiza kuwa uamuzi wa kujiunga na CCM umetokana na hiari yake mwenyewe, akikanusha taarifa zinazodai kuwa alipewa fedha ili ahame chama.

"Nimejiunga na CCM kwa ridhaa yangu mwenyewe na nikiwa na akili timamu. Taarifa kwamba nimelipwa fedha ili nihame chama si za kweli," alieleza.

Jumbe pia alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abrahman Abdallah, kwa ushirikiano aliompatia hadi kufanikisha uamuzi wake wa kujiunga na chama hicho, huku akimpongeza kwa juhudi zake za kuimarisha CCM mkoani humo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, alisema kujiunga kwa Jumbe ni faida kubwa kwa chama kutokana na uzoefu na ushawishi aliokuwa nao katika siasa za upinzani.

"Mkizungumza kuhusu upinzani Wilaya ya Tanga, baba yake ni Rashid Hamza Jumbe. Wanachama wa CCM ni mashahidi; kila tuliposikia kuna mkutano wa CHADEMA tulijua Rashid anakuja kutupa wakati mgumu. Leo ameamua kujiunga na CCM," alisema.

Aliongeza kuwa hatua ya Jumbe kuhamia CCM ni ishara ya kuendelea kudhoofika kwa upinzani katika Mkoa wa Tanga, akieleza kuwa atakuwa sehemu ya kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم