TAMASHA KUBWA LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTALII KUTIKISA ARUSHA,ARUSHA ARTISAN FESTIVAL KUFUNGUA FURSA MPYA ZA AJIRA NA UWEKEZAJI

 ARUSHA KUWA KITOVU CHA TAMASHA KUBWA LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTALII

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

MKOA wa Arusha unatarajiwa kuwa kitovu cha sanaa, utamaduni na utalii mwezi Oktoba mwaka huu baada ya zaidi ya washiriki 2,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania kuthibitisha kushiriki Tamasha la Kimataifa la Arusha Artisan Festival, litakalolenga kuitangaza Tanzania kupitia uchumi wa ubunifu, kuongeza ajira kwa vijana na kupanua soko la kimataifa la kazi za sanaa.

Waandaaji wa tamasha hilo wamesema litakuwa la kwanza nchini kuunganisha kwa kiwango kikubwa sekta za utalii, sanaa na utamaduni kupitia maonesho ya wazi (outdoor festival), warsha za kitaalamu, mafunzo ya ujasiriamali, mijadala, maonesho ya ubunifu na utoaji wa tuzo kwa wasanii.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othuman Jama, alisema tamasha hilo litawakutanisha wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mitindo, wafinyanzi, wafumaji, wajasiriamali, wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali.

Akiongea na waandishi wa habari mapema leo Julai 3,2026,alisema lengo kuu ni kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa sanaa na utamaduni huku likiwajengea vijana maarifa, uwezo na fursa mpya za kiuchumi.

"Hili si tamasha la biashara pekee, bali ni jukwaa la elimu, ubunifu na maendeleo endelevu. Tunataka sanaa iwe sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii," alisema Jama

Aliongeza kuwa taasisi mbalimbali zikiwemo SIDO, TEMDO na BASATA pamoja na wadau wa sekta ya utalii na utamaduni zitashiriki ili kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa ubunifu.

Kwa mujibu wa Jama, tamasha hilo pia litaweka msingi wa kutambua na kuhesabu wasanii wa sanaa nchini ili kuwawezesha serikali na wadau kupanga mikakati bora ya kuendeleza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Rukia Walele, alisema tamasha hilo limefungua ukurasa mpya wa kuitangaza sekta ya sanaa za ufundi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikichangia uchumi na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania bila kupata utambuzi unaostahili.

Alisema TAFCA linaunganisha zaidi ya vyama 20 vya sanaa za ufundi nchini vinavyohusisha wachongaji, wachoraji, wafinyanzi, wafumaji, watengenezaji wa bidhaa za ngozi, wabunifu wa mavazi, wataalamu wa urembo na makundi mengine ya kazi za mikono.

"Sanaa za ufundi ndiyo msingi wa sekta nyingi za ubunifu. Tamasha hili litawafungulia wasanii wetu masoko mapya, kuongeza kipato na kuitangaza Tanzania kupitia kazi za mikono," alisema Walele.

Naye Mshauri wa Kiufundi wa Arusha Artisan Festival, Andrew Bumba, alisema tamasha hilo litakuwa kichocheo cha ajira kwa maelfu ya vijana kwa kuwaunganisha moja kwa moja na sekta ya utalii pamoja na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alisema waandaaji wamejipanga kutumia mifumo ya kidijitali kuwaunganisha wasanii na wanunuzi, huku tamasha hilo likitekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kupunguza umaskini, kukuza ubunifu na kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa kiwango kikubwa.

"Tunataka kuona wasanii wetu wanafanya kazi katika mfumo rasmi, wanapata masoko ya uhakika na kunufaika na huduma za kifedha ili sanaa iwe chanzo kikubwa cha ajira na mapato ya taifa," alisema Bumba.

Ofisa wa Timu ya Media wa Tanzania Tourism Festivals, Joseph Rumanyika, alisema tamasha hilo pia litatumika kutoa elimu ya utalii kwa wananchi na kuwaunganisha wasanii na fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Alisema Arusha imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake kama kitovu cha utalii nchini na lango la vivutio vya mzunguko wa kaskazini (Northern Circuit), hali itakayowapa wageni nafasi ya kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya utalii sambamba na kushiriki maonesho ya sanaa.

"Tunataka kuwafikia wasanii wengi zaidi kwa elimu na kuwaunganisha na masoko ya ndani na kimataifa kupitia utalii. Hili ni jukwaa la kuonyesha kuwa sanaa inaweza kuwa injini muhimu ya maendeleo ya uchumi," alisema Rumanyika.

Waandaaji wanaamini tamasha hilo litafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya sekta ya utalii na sanaa, kuongeza idadi ya watalii, kuvutia uwekezaji, kuongeza mauzo ya bidhaa za ubunifu na kuifanya Arusha kuwa kitovu cha matukio makubwa ya kimataifa yanayotangaza Tanzania kupitia sanaa, utamaduni na utalii.





Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم