SIMBA YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA, YAWAFUTA KAZI WACHEZAJI SABA AWA HAPA KUELEKEA MSIMU MPYA

SIMBA YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA, YAWAAGA WACHEZAJI SABA KUELEKEA MSIMU MPYA

Na Joseph Ngilisho-Arushadigital 

KLABU ya Simba SC imeanza rasmi mchakato wa kukisuka upya kikosi chake kuelekea msimu wa mashindano wa 2026/27 baada ya kutangaza kuachana na wachezaji saba, hatua inayotafsiriwa kama sehemu ya mageuzi makubwa ya kuimarisha ushindani wa timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram leo Julai 16, 2026, imeambatana na neno "ASANTENI", pamoja na picha za wachezaji wanaoondoka, huku ikieleza kuwa taarifa zaidi kuhusu uamuzi huo zitatolewa kupitia majukwaa rasmi ya mawasiliano ya Simba.

Wachezaji waliomaliza safari yao ndani ya kikosi hicho ni Chamou Karaboue, Naby Camara, Edwin Balua, Joshua Mutale, Awesu Awesu, Omari Omari na Moussa Camara.

Uamuzi huo unaashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa ndani ya kikosi cha Simba, ambacho kinatarajiwa kufanyiwa maboresho katika maeneo mbalimbali ili kuongeza ushindani wa timu hiyo katika msimu ujao.

Baadhi ya nyota walioondoka walikuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na michuano ya kimataifa katika msimu uliopita, wakitoa mchango wao kwa nyakati tofauti kabla ya uongozi kuamua kutovunja mkataba au kutowaongezea mikataba mipya.

Hatua hiyo inaongeza kasi ya maandalizi ya Simba kuelekea msimu mpya, huku mashabiki wakisubiri kuona ni wachezaji gani wapya watakaosajiliwa kuziba nafasi zilizoachwa na walioondoka na kuongeza nguvu katika harakati za kutwaa mataji ya ndani na kufanya vizuri zaidi kimataifa.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم