SHEIKH HARUNA APIGA MKWARA,ATAKA KAULI ZA UCHOCHEZI ZIKOME,AITA MARIDHIANO KWA WANASIASA

VIONGOZI WA DINI WATAKA KAULI ZA UCHOCHEZI ZIKOME, WASISITIZA MARIDHIANO YA KISIASA

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

Kiongozi wa Dini wa Taasisi ya Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya Tanzania, Sheikh Haruna Husein, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuachana na kauli za uchochezi na badala yake kuweka mbele maridhiano, mazungumzo na amani kwa maslahi ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Zawia kuu Arusha, Sheikh Haruna alisema msimamo wake kuhusu umuhimu wa viongozi kukaa meza moja kutafuta suluhu ya tofauti za kisiasa si wa leo, kwani alianza kuueleza hadharani tangu Agosti 23 mwaka jana na anaendelea kuusisitiza.

Alisema suluhisho la tofauti za kisiasa haliwezi kupatikana kupitia mijadala ya mitandaoni au matamshi makali ya viongozi, bali kwa mazungumzo ya heshima yanayojengwa katika misingi ya subira, upole, ukarimu na uchamungu kama yanavyofundishwa na dini.

"Kauli za uchochezi hazijengi Taifa. Tunahitaji viongozi wakae meza moja, wazungumze na kutafuta maridhiano kwa maslahi ya Watanzania wote," alisema.

Aliongeza kuwa migogoro ya kisiasa huwaathiri zaidi wananchi wa kawaida wanaopambana na changamoto za maisha, hivyo viongozi wanapaswa kutanguliza ustawi wa Taifa badala ya maslahi binafsi au ya kisiasa.

Sheikh Haruna alisema hatua zozote zinazowakutanisha viongozi kwa ajili ya kujenga maridhiano zinapaswa kuungwa mkono na kupongezwa kwa kuwa zinaimarisha umoja wa kitaifa na kulinda amani ambayo Tanzania imeendelea kujivunia kwa miaka mingi.

Akizungumzia mikutano ya kisiasa, alisema shughuli hizo zinapaswa kufanyika katika mazingira ya amani, kuheshimiana na kuzingatia sheria za nchi ili kulinda mshikamano wa kitaifa.

Aliwataka pia viongozi wa vyama vya siasa kubadili lugha wanazotumia wanapowahutubia wananchi, akisisitiza kuwa kauli zenye staha na busara zitasaidia kujenga mazingira ya utulivu kuelekea katika mustakabali mwema wa nchi.

"Ninatoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa waachane na kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko. Tujenge umoja, tushikamane na tuweke mbele maridhiano ili Tanzania iendelee kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika," alisema Sheikh Haruna.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم