SERIKALI YAAGIZA MAPAMBANO MAKALI DHIDI YA KIPINDUPINDU, YALENGA TANZANIA ISIWE NA KISA HATA KIMOJA

SERIKALI YAAGIZA MAPAMBANO MAKALI DHIDI YA KIPINDUPINDU, YALENGA TANZANIA ISIWE NA KISA HATA KIMOJA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

SERIKALI imeagiza maofisa afya katika mikoa na halmashauri zote nchini kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira ili kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la kutokuwa na kisa hata kimoja cha ugonjwa wa kipindupindu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathmini ya utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira kwa ngazi ya mikoa na halmashauri za Tanzania Bara uliofanyika jijini Arusha.

Prof. Shemdoe alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja cha kudhibiti mlipuko wa kipindupindu yanapaswa kuwa chachu ya kufikia hatua ya kutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini.

Alisisitiza kuwa ili kufikia lengo hilo, ni lazima sekta ya afya iendelee kuimarishwa sambamba na usafi wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kuendelea kuchukua hatua za haraka za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya milipuko kabla hayajasambaa.

"Tunahitaji kuongeza juhudi zaidi hadi kufikia hatua ya kutokuwa na kisa hata kimoja cha kipindupindu nchini. Hii itafanikiwa kwa kuimarisha huduma za afya, usafi wa mazingira na utekelezaji wa hatua madhubuti za kudhibiti magonjwa ya milipuko ili kulinda afya za wananchi," alisema.

Katika kuimarisha usalama wa chakula, Waziri huyo alisema hadi kufikia Mei mwaka huu, jumla ya wazalishaji na wauzaji wa chakula 813 walikuwa wamekaguliwa, huku wazalishaji 29 wakisajiliwa na kufanya idadi ya waliosajiliwa kufikia 545 tangu mwaka wa fedha 2024/2025.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka maofisa afya nchini kuhakikisha wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wote wa chakula wanaendelea kusajiliwa na kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha vyakula vinavyowafikia wananchi vinazingatia viwango vya usalama na ubora.

Katika hatua nyingine Shemdoe aliwaagiza Wakuu wote wa Mikoa ya Tanzania bara kusimamia na kurejesha kampeni za ufanyaji wa usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi ili kuondoa magonjwa ya milipuko kwenye jamii.

"Wakuu wa Mikoa oneni namna mtakavyoshusha maelekezo haya kwenye Wilaya zetu, kwenye Halmashauri zetu, Tarafa, Kata, Vijiji na Vitongoji vyetu ili kuimarisha hali ya usafi kwenye maeneo yetu." Alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dk. Rashid Mfaume, alisema mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa afua mbalimbali za afya ya mazingira nchini.

Alieleza kuwa tathmini hiyo inajumuisha hali ya upatikanaji na matumizi ya vyoo bora katika kaya, taasisi za elimu, vituo vya kutolea huduma za afya na maeneo ya umma, pamoja na utekelezaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kujikinga dhidi ya magonjwa yanayotokana na mazingira yasiyo salama.

Aidha, alisema wataalamu hao pia wanapima kiwango cha utayari wa taifa kukabiliana na magonjwa hatari ya milipuko ambayo yanaweza kuingia nchini wakati wowote, ikiwemo Ebola, pamoja na Dengue, Malaria na magonjwa mengine yanayoweza kuhatarisha afya ya jamii endapo hatua za tahadhari hazitachukuliwa mapema.

Naye Mratibu wa Mradi Endelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP), Seleman Londo, alisema serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta ya afya, maji na usafi wa mazingira kwa kuongeza idadi ya kaya zinazotumia vyoo bora na salama.

Alisema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kupunguza magonjwa yanayosababishwa na mazingira machafu na kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama yenye kuzingatia afya na ustawi wa jamii.



Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم