DEREVA WA MAKAMU MWENYEKITI CHADEMA AFARIKI AKIWA GESTI KIGOMA
By Arushadigital-KIGOMA
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Amani Golugwa, ametangaza kifo cha Swezi Dani Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche.
Maradufu amefariki dunia leo, Julai 1, 2026, baada ya kukutwa akiwa hana uhai ndani ya chumba alichokuwa amefikia katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Golugwa alisema wasiwasi ulianza mapema asubuhi baada ya Maradufu kushindwa kufika kumchukua John Heche kama ilivyokuwa kawaida katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Alisema baada ya juhudi za kumpigia simu mara kadhaa kugonga mwamba, viongozi wa CHADEMA waliamua kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kutokana na hofu waliyoanza kuwa nayo.
Kwa mujibu wa Golugwa, askari polisi walifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni na, baada ya kushirikiana na wahusika wa eneo hilo, walivunja mlango wa chumba alichokuwa amefikia na kumkuta tayari amefariki dunia.
Golugwa amesema mwili wa marehemu umechukuliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya uchunguzi, huku chanzo cha kifo kikisubiri kubainishwa kupitia uchunguzi wa kitaalamu unaoendelea.
Amesisitiza kuwa CHADEMA inasubiri taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi na wataalamu wa afya kuhusu chanzo halisi cha kifo hicho, huku akitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wanachama wa chama hicho walioguswa na msiba huo.
**ends**

إرسال تعليق