MKOPO WA SH. BILIONI 200 KUWAINUA VIJANA KIUCHUMI – NANAUKA
Na Joseph Ngilisho, Arusha
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha jitihada za kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kupitia Programu ya Mikopo ya Shilingi Bilioni 200 ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana inayotekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya CRDB.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati wa uzinduzi rasmi wa utoaji wa mikopo hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Nanauka alisema programu hiyo inalenga kuwawezesha vijana wenye miradi yenye tija kupata mtaji wa kuanzisha, kuendeleza na kupanua shughuli zao za kiuchumi, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara, kuimarisha uchumi wa Taifa na kufungua nafasi mpya za ajira kwa vijana wengine.
Alisema Serikali imeamua kuwekeza katika vijana kwa kutambua kuwa ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa, hivyo kuwawezesha kifedha kutachochea ubunifu, ujasiriamali na ushindani katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Katika hafla hiyo, vikundi vitatu vya vijana kutoka Mkoa wa Arusha vilikabidhiwa mikopo yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 730, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mikopo ya Shilingi Bilioni 200 ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Waziri Nanauka alisema mikopo hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwawezesha vijana kuanzisha na kukuza miradi yenye tija, kuongeza thamani ya bidhaa na huduma, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa.
Aidha, aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, kuisimamia kwa uadilifu na kuhakikisha inaleta matokeo chanya ili mfuko huo uweze kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.
"Pia nawahimiza vijana wengine kujitokeza na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kupitia programu hii na nyinginezo, kwani ni njia muhimu ya kujenga uchumi binafsi, kuondokana na utegemezi na kuchangia maendeleo ya Taifa," alisema Nanauka.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kifedha kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata mitaji nafuu na fursa zinazowawezesha kuwa wabunifu, wazalishaji na waajiri badala ya kutegemea ajira pekee.
Ends.





إرسال تعليق