KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ACHARUKA, AITAKA TARURA KUONDOA KERO YA VUMBI ARUMERU

 TARURA YAAGIZWA KUMALIZA KERO YA BARABARA BWAWANI

Na Joseph Ngilisho | Arusha

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, ameuagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Arumeru kuchukua hatua za haraka kuboresha barabara ya Kata ya Bwawani, Halmashauri ya Arusha, ili kuondoa kero ya vumbi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Mwang'onda alitoa agizo hilo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Bwawani, mradi wa utawala bora wenye thamani ya shilingi milioni 84.4, uliojengwa kupitia michango ya wananchi, wadau wa maendeleo na baadaye kukamilishwa kwa fedha za Serikali.

Alisema Serikali imepokea malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara hiyo, ambao umekuwa ukisababisha vumbi na usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo, hivyo TARURA inapaswa kuanza maboresho ya haraka wakati maandalizi ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha kisasa yakiendelea.

"Ni muhimu wananchi wa Bwawani waanze kunufaika na miundombinu bora. TARURA ihakikishe changamoto hii inapatiwa ufumbuzi wa haraka," alisema Mwang'onda.

Sambamba na hilo, aliwapongeza wananchi wa Kata ya Bwawani kwa uzalendo na mshikamano wao katika kuchangia ujenzi wa ofisi hiyo, akisema ushiriki wao umeonyesha namna nguvu za wananchi zinavyoweza kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wananchi zinazolenga kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha utawala bora katika ngazi za msingi.

Baada ya uzinduzi wa mradi huo, Mwang'onda, wakimbiza Mwenge wa Uhuru pamoja na viongozi mbalimbali walishiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la ofisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ends.

Post a Comment

أحدث أقدم