MENO YALIYOTOBOKA YATAWALA KATIKA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA KAMBI YA SELIANI SELIANI,WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA MATIBABU BURE

MENO YALIYOTOBOKA YATAWALA KWA WAGONJWA WALIOFIKA KAMBI YA SELIANI

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

DAKTARI wa Kinywa na Meno wa Halmashauri ya Arusha DC, Dkt. Esther Luhonga, amesema wagonjwa wengi waliojitokeza katika siku ya kwanza ya kambi ya madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno inayofanyika katika Hospitali ya Seliani wamebainika kuwa na tatizo la meno yaliyotoboka pamoja na magonjwa ya fizi.

Dkt. Luhonga alisema leo julai 23, katika siku ya kwanza ya kambi hiyo, wagonjwa 33 walipatiwa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya kinywa na meno.

Alisema huduma zinazotolewa zinategemea tatizo la mgonjwa, ikiwemo kuziba meno yaliyotoboka, kung'oa meno yasiyoweza kutibika, pamoja na kusafisha fizi kwa wenye magonjwa ya fizi.

"Kwa mgonjwa mwenye jino lililotoboka ambalo linaweza kutibika tunaliziba, na kama haliwezi kutibika tunaliondoa. Wenye magonjwa ya fizi wanapatiwa huduma ya kusafishwa fizi ili kuondoa tatizo," alisema.

Aliongeza kuwa mbali na matibabu, wananchi wanapatiwa elimu ya kujikinga na magonjwa ya kinywa na meno, ikiwemo matumizi sahihi ya mswaki na umuhimu wa kupiga mswaki kwa usahihi ili kuzuia kuoza kwa meno.

Dkt. Luhonga alisema kambi hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano na timu ya madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno wakiongozwa na daktari bingwa kutoka Ujerumani, ambapo wananchi wanapata huduma zote muhimu kulingana na mahitaji yao.

Aliwataka wananchi ambao hawakufika siku ya kwanza kutumia fursa ya siku ya pili kufika Hospitali ya Seliani kwa ajili ya uchunguzi, elimu na matibabu ya bure.

"Ninawaalika wananchi wote wa Arusha DC wafike Hospitali ya Seliani. Bado tunaendelea kutoa huduma kesho, hivyo waje wapate uchunguzi, elimu na matibabu ya magonjwa ya kinywa na meno," alisema.

Akizungumzia hali ya huduma katika Halmashauri ya Arusha DC, Dkt. Luhonga alisema huduma za afya ya kinywa na meno zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma, huku wataalamu wakiendelea kuwahudumia wananchi wanaohitaji matibabu.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post