LUKUMAY AKERWA NA WATAALAMU KUTOTAMBUA MRADI WA ZAHANATI YA KIJIJI CHA ENGUTOTO, AAGIZA TAARIFA YA HARAKA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameonyesha kutoridhishwa na kushindwa kwa baadhi ya wataalamu wa Halmashauri ya Arusha kutambua uwepo wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Engutoto, unaotekelezwa kwa nguvu na michango ya wananchi.
Dkt. Lukumay alitoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 17,2026 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo,kujitambulisha na kuwashukuru wananchi kwa kumchagua katika Kata ya Mwandeti, ambapo alifika katika eneo la ujenzi wa zahanati hiyo na kukuta mradi ulioanzishwa mwaka 2017 ukiwa haujakamilika kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wake.
Akiwa katika eneo la mradi, mbunge huyo alimtaka mganga mkuu wa hlamashauri ya Arusha(DMO),aliyewakilishwa na Butolwa Bujiku na Mkuu dara ya Mipango na uratibu wa Halmashauri hiyo Norasko Kaitira kueleza hatua iliyofikiwa na sababu za kuchelewa kukamilika kwa zahanati hiyo. Hata hivyo, alielezwa kuwa wataalamu hao hawakuwa na taarifa kuhusu uwepo wa mradi huo.
Majibu hayo yalimkera Dkt. Lukumay, ambaye alisema ni jambo lisilokubalika kwa wataalamu wanaosimamia sekta muhimu kushindwa kufahamu miradi inayotekelezwa ndani ya halmashauri yao, hususan ile inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi.
"Haikubaliki kabisa wataalamu kutofahamu mradi ambao wananchi wameuchangia kwa nguvu zao. Hii inaonyesha kuna udhaifu mkubwa katika ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo," alisema.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Lukumay aliagiza apelekewwe kwa haraka taarifa ya kina kuhusu mradi huo ikieleza historia yake, hatua iliyofikiwa, fedha zilizokwisha kutumika, changamoto zilizousababisha kusuasua pamoja na mpango wa kuukamilisha.
Mbali na agizo hilo, mbunge huyo alimuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha pamoja na wakuu wote wa idara kuhakikisha wanashuka mara kwa mara vijijini kukagua na kusimamia miradi ya maendeleo badala ya kutegemea taarifa zinazowasilishwa ofisini.
Alisema usimamizi wa karibu utasaidia kubaini changamoto mapema, kuongeza uwajibikaji wa watendaji na kuhakikisha fedha zinazowekezwa kwenye miradi ya maendeleo zinatoa thamani kwa wananchi.
"Viongozi na wataalamu hawawezi kusimamia maendeleo kwa kukaa ofisini pekee. Lazima washuke vijijini kuona hali halisi ya miradi, kusikiliza wananchi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo," alisema Dkt. Lukumay.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Engutoto, Jonas Mollel, alisema ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2017 kwa nguvu za wananchi waliolenga kusogeza huduma za afya karibu na makazi yao.
Alisema pamoja na wananchi kujitolea nguvu kazi na kuchangia rasilimali mbalimbali, mradi huo umeshindwa kukamilika kutokana na uhaba wa fedha na ukosefu wa ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa wataalamu wa halmashauri.
Wananchi wa Engutoto walieleza matumaini yao kuwa ziara ya Dkt. Lukumay na maagizo aliyoyatoa yatachochea hatua za haraka za kukamilisha zahanati hiyo ili ianze kutoa huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo jirani.
Katika hatua nyingine Lukumay alitembelea pia mradi wa ujenzi wa jengo la Hostel ya wasichana katika shule ya sekondari Engawalet ambalo ujenzi wale unagharibu kiasi cha sh,milioni 110 ,litakalo chukua wanafunzi wa kike kati ya 48 hadi 52
Miradi hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa miradi ambayo wananchi wamewekeza nguvu na rasilimali zao kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hivyo wakisisitiza kuwa unahitaji usimamizi wa karibu na msukumo wa Serikali ili ukamilike kwa manufaa ya jamii.
Ends







إرسال تعليق